
Bonface Mwangi Kariuki, mchuuzi aliyepigwa risasi kwa karibu wiki mbili zilizopita wakati wa maandamano jijini Nairobi, amefariki dunia, msemaji wa familia Emily Wanjira amesema alifariki saa 9:15 alasiri.
Muuzaji huyo wa barakoa mwenye umri wa miaka 22 aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi kichwani kwa karibu wakati wa maandamano ya "Haki kwa Albert Ojwang" ametangazwa kuwa amefariki ubongo (brain dead) siku ya Jumapili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) siku ya Jumapili, msemaji wa familia Emily Wanjira alisema madaktari waliwataarifu kuwa shina la ubongo la Kariuki lilikuwa limekoma kufanya kazi, ingawa moyo wake bado ulikuwa unapiga kwa msaada wa mashine.
Kariuki alipigwa risasi mnamo Juni 17 katika Barabara ya Tom Mboya jijini Nairobi wakati wa maandamano yaliyotaka Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat ajiuzulu kufuatia kifo cha mtangazaji wa mitandaoni Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi.
Video iliyosambaa sana mtandaoni ilionyesha maafisa wawili wa polisi wakimkabili Kariuki kabla ya mmoja wao kumpiga risasi kwa karibu na kumwacha bila fahamu.
Tangu wakati huo, Kariuki amefanyiwa upasuaji mgumu mara tatu katika KNH ambako amekuwa akihifadhiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Madaktari waliondoa kitu kama risasi kilichokuwa kimekwama kwenye ubongo wake, ambacho Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt William Sigilai, alisema huenda kilikuwa risasi ya mpira — ingawa uchunguzi wa kitaalamu bado unaendelea.
Licha ya upasuaji huo, vipande vya risasi bado vipo kwenye ubongo wake, na madaktari wamesema hakuna tena shughuli yoyote ya ubongo. Kariuki amekuwa akitegemea mashine kuendelea kuishi kwa karibu wiki mbili.
“Alifanyiwa upasuaji mwingine Ijumaa ambapo mirija ya kupumua ilihamishwa kutoka puani hadi kooni,” Wanjira alieleza. “Pia alifanyiwa utaratibu wa kupachika bomba la chakula moja kwa moja tumboni kwa kuwa hakuweza tena kumeza.”
Familia imesema bili ya hospitali sasa imevuka Shilingi milioni 3. Wameomba msaada kutoka kwa wahisani huku wakijiandaa kwa hali yoyote itakayofuata.
Baba yake Kariuki, Jonah Kariuki, alieleza uchungu wake na kukosoa ukosefu wa haki.
“Ubongo wa mwanangu haufanyi kazi tena, lakini moyo wake bado unapiga. Tunahitaji msaada kulipia gharama,” alisema.
Katika hali iliyozidisha machungu yao, familia ilifichua kuwa walidanganywa Shilingi 200,000 na mtu aliyedai kuwasaidia kupanga matibabu.
Kisa cha kupigwa risasi kwa Kariuki kimezua hasira kote nchini, huku mashirika ya haki za binadamu yakitoa wito kwa polisi kuwajibishwa.
Amnesty International imemtaja Kariuki miongoni mwa waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano yanayoongozwa na kizazi cha Gen Z, ambayo tayari yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 16 na wengine zaidi ya 400 kujeruhiwa kote nchini, wengi wao wakidaiwa kupigwa risasi na polisi.