
Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani, Dkt. Fred Matiang’i, amepuuzilia mbali madai kwamba yeye ni mradi wa kisiasa wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.
Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne usiku, Matiang’i alisema kwamba hajajiunga na chama chochote cha kisiasa na bado anashauriana na viongozi kutoka pande zote za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Matiang’i, ambaye aliwahi kuhudumu katika wizara tatu chini ya utawala wa Kenyatta, alikanusha madai kwamba uhusiano wake wa karibu wa kikazi na rais huyo wa zamani unamfanya kuwa kikaragosi, akisema madai hayo hayana msingi.
“Uhuru aliteua takriban mawaziri 30. Wengine bado wanahudumu hadi leo. Je, mimi ni mradi kwa sababu nilikuwa kwenye baraza lake la mawaziri? Kama ni suala la kuhudumu, basi je, nitaitwa pia mradi wa Benki ya Dunia?” alihoji.
Aidha, alifafanua kwamba hajawahi kuomba uungwaji mkono kutoka kwa Kenyatta kwa ajili ya kuwania urais, ingawa bado wako na mawasiliano na wakati mwingine huzungumzia masuala ya kitaifa.
Matiang’i pia alisisitiza haja ya umoja na uundaji wa miungano ya kisiasa, akibainisha kuwa hali ya sasa ya kisiasa haiwezekani kuruhusu chama kimoja kushinda mamlaka pekee.
“Utasikia wengine wakijinasibisha na mimi... lakini nataka kushiriki katika majadiliano ya kina na jumuishi kabla ya kuamua chombo cha kisiasa,” alisema, akifichua kuwa tayari ameendesha mazungumzo na vyama 7 hadi 8 kufikia sasa.
Kauli zake zinakuja kufuatia ripoti za hivi majuzi kuwa Chama cha Jubilee kimemuidhinisha kuwa mgombea wake wa urais – hatua ambayo imezua hisia kuwa Kenyatta ana ushawishi katika uwezekano wa Matiang’i kuwania urais.