
Wabunge wanaounga mkono chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wamemtahadharisha Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua kuacha kumzungumzia vibaya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Wabunge hao pia wamemtaka kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens kumheshimu Rais William Ruto.
Mbunge wa Ruaraka, Tom Kajwang’, alisema Gachagua anaonekana mwenye chuki baada ya kuondolewa kwenye wadhifa wake wa naibu rais, na akasisitiza kuwa anapaswa kuukubali ukweli wa hali yake ya sasa.
“Lazima ana matatizo yanayotokana moja kwa moja na kuondolewa kwake madarakani. Anapaswa kukubali ukweli kwamba hawezi tena kushikilia wadhifa wowote wa umma,” alisema Kajwang’.
“Tunajua kuwa mlango ulifungwa siku Seneti ilipopiga kura ya kumwondoa. Hata akijaribu kuufungua kwenye korido, mahakamani au hadharani, hataweza. Lazima akubali hilo,” aliongeza.
Mbunge wa Kisumu Central, Joshua Oron, alimkumbusha Gachagua kuwa Raila Odinga amekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu zaidi na hivyo anastahili kuheshimiwa.
Alisema Raila na Gachagua hawawezi kuwekwa kwenye kiwango kimoja cha kisiasa.
“Gachagua sio sawa na Raila Odinga kisiasa. Uhuru wa kujieleza anaoufurahia leo ulipiganiwa na Raila. Katiba anayoinufaika nayo leo Gachagua ilipiganiwa na Raila,” alisema Oron.
“Hivyo basi, Gachagua anapaswa kuacha na kuondoa jina la Raila mdomoni mwake. Kumzungumzia vibaya Raila na Rais Ruto hakutabadilisha Kenya kwa njia yoyote ile,” aliongeza.