
Gavana wa Kisii Simba Arati amemhimiza Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kumuunga mkono aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, katika azma yake ya kuwania urais.
Akizungumza siku ya Jumatano, Julai 2, 2025, Arati alisema kuwa iwapo Raila atamtangaza hadharani Matiang’i, huenda akawa rais ajaye.
Aidha, alisema hana pingamizi endapo Rigathi Gachagua, au hata William Ruto, wataamua kumuunga mkono Matiang’i, akisisitiza kuwa jamii ya Gusii itasimama na Matiang’i katika safari hiyo.
Arati aliongeza kuwa waziri huyo wa zamani atakuwa sehemu ya timu itakayounda serikali ijayo.
“Matiang’i atakuwa kwa hiyo meza ya kutengeneza serikali kuu ya nchi hii, lakini hatutaki mtu atoke kule ooh lazima kwa sababu nimesikia wamejipanga walikuwa wafanye mkutano hapa leo, ooh tufanye mkutano Kisii tualike Matiang’i, Matiang’i ndio anaalika wewe,” alisema.
“Nataka kuambia Gachagua kama utashika ndugu yetu mkono hatuna shida, William Ruto kama utashika Matiang’i mkono useme tosha hatuna shida, ata mzee Raila nataka kumwambia ya kwamba akisema unajua yeye ndio ataamua hii Kenya ikuwe namna gani sasa tunaomba baba vile tunaenda juu lazima tukuwe katika serikali ijayo.”
Pia aliwasihi wakazi kudumisha amani.
“Na nataka kuwaomba watu wa Kisii tukuwe na amani watu wakija, tuwape masikio waonge, lakini kura yako iko, kusikuwe na fujo yoyote,” alisema.
Kauli za Arati zinajiri baada ya baadhi ya viongozi wa eneo la Gusii kutangaza hadharani kumuunga mkono Matiang’i kwa urais.
Wakiongozwa na Seneta wa Kisii Richard Onyonka, viongozi hao ni pamoja na Seneta wa Nyamira Omukongo Omogeni, Mbunge wa Nyaribari Masaba Daniel Manduku, Mbunge wa Kitutu Masaba Gesairo Clive, Seneta Mteule Gloria Orwoba, na Mbunge wa Kitutu Chache Japheth Nyakundi, waliandaa kikao cha kifungua kinywa na Matiang’i.
Katika taarifa siku ya Jumatano, Julai 2, 2025, Seneta Onyonka alisema kuwa waziri huyo wa zamani amejitolea kwa uongozi wa mageuzi nchini.
“Nilipata heshima kuhudhuria kikao cha kifungua kinywa cha baadhi ya viongozi wa Gusii kilichoandaliwa na Fred Matiang’i. Matiang’i amejitolea kushiriki katika uongozi wa maendeleo na mageuzi nchini!” alisema.
Haya yanajiri siku moja baada ya Matiang’i kukanusha madai kwamba azma yake ya urais inaendeshwa na watu wenye ushawishi nyuma ya pazia.
“Sidhani kwamba hilo ni jambo la kujadiliwa hadharani. Ukweli ni kwamba unapojitosa kwenye kampeni, unatafuta wafadhili na watu wa kukuunga mkono katika kampeni,” alisema.