
Naibu Rais Kithure Kindiki amemshambulia vikali mtangulizi wake Rigathi Gachagua kwa kile alichokitaja kuwa ni kupenda sana kujadili sauti yake.
"Halafu wengine wanaongea mambo yetu hapo na ni watu bure hata hawana akili. Naskia akisema ati huyo Kindiki anaongea na soprano. Wewe mwanaume unaongelea kuhusu sauti ya mwanaume mwenzako, kwani uko na nia gani wewe?
"Wale ambao wameruhusiwa kuzungumza kuhusu mambo ya wanaume ni wanawake pekee yao. Sasa wewe mwanaume unajadili mambo ya mwanaume mwenzako, kwani wewe ni mwanaume aina gani?"
Kindiki alitoa kauli hiyo katika eneo la Langobaya, eneobunge la Malindi, katika kaunti ya Kilifi siku ya Jumatano.
Aliwataka Wakenya kuwapuuza viongozi ambao hawana ajenda nyingine zaidi ya kueneza kauli za "muda wa kipindi kimoja" na "Ruto lazima aondoke!"
"Kuna watu ambao kazi yao ni kuongea kuhusu 'team ya Kasongo' na one term. Wakiulizwa ni nini watafanya vizuri, mfumo gani utakaobadilisha, wanasema one term. Kwa hivyo wale majamaa watukome na wakome wananchi," alisema Kindiki.
"Wengine hapo walishindwa na kazi. Walipewa kazi kubwa ikawashinda. Hawajui kukaa vizuri na wananchi, hawajui kukaa vizuri na viongozi wenzao. Sasa wanarandaranda huko wakiongea mambo ya upuzi, kama wendawazimu," aliongeza.
Naibu Rais alisema serikali imejizatiti kuhakikisha maendeleo ya usawa na kuwawezesha Wakenya kiuchumi kupitia sera, programu na miradi ya mageuzi.
"Katika Kaunti ya Kilifi na kaunti nyingine za Pwani na Nyanza, tunajenga maeneo ya kushukia samaki na kuyawezesha kwa vifaa vya kisasa ili kuimarisha uzalishaji wa samaki na kuongeza thamani ya bidhaa zao kwa ajili ya kuinua uchumi wa wavuvi," alisema.
"Serikali tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 3.2 kama ruzuku kwa wavuvi kupitia vikundi vyao vya Beach Management Units (BMUs) ili kuchochea biashara zao. Tuko katika hatua za mwisho za kununua mashua za uvuvi wa bahari kuu ili kuongeza uzalishaji wa samaki," aliongeza.
Kindiki alisema kuwa katika mpango unaoendelea wa kuunganisha umeme hadi ngazi ya mwisho nchini, jumla ya kaya 20,000 zaidi katika Kaunti ya Kilifi zitaunganishwa na gridi ya taifa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.8.
"Shilingi milioni 132 zimetengwa kwa ajili ya Eneobunge la Malindi ili kuunganisha kaya 2,200 mpya," aliongeza.
Waliokuwepo katika hafla hiyo ni pamoja na Salim Mvurya (Waziri wa Michezo), Gideon Mung'aro (Gavana, Kilifi), Abdulswamad Nassir (Gavana, Mombasa) na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah.