
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimekashifu ripoti za vyombo vya habari zilizodai kuwa umaarufu wa kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga, unazidi kupungua katika ngome yake ya Nyanza.
Hii inajiri baada ya baadhi ya waliokuwa wamehudhuria mazishi ya mwanablogu Albert Ojwang huko Homa Bay kueleza kutoridhishwa kwao na ushirikiano wa Raila na Rais William Ruto kupitia mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Katika taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa kitaifa wa ODM, Gladys Wanga, chama hicho kilikanusha madai hayo, kikieleza kuwa mazishi hayo yalikuwa tukio la kitaifa lililohudhuriwa na watu kutoka itikadi mbalimbali za kisiasa.
“Ilikuwa ni hafla iliyovuta wahudhuriaji kutoka kila pembe ya nchi, kutoka Pwani ambako Albert alisoma na kufanya kazi, hadi Nairobi ambako alifariki akiwa mikononi mwa polisi, na hatimaye Homa Bay, nyumbani kwao kwa mababu,” Wanga alisema.
“Hisia za waombolezaji zilikuwa dhahiri, lakini ibada na mazishi yalifanyika kwa amani, kinyume na matarajio ya machafuko.”
Chama hicho kilisisitiza kuwa mchango wa Raila katika historia ya taifa hauwezi kupuuzwa, kikitaja msimamo wake wa kudumu katika kupigania haki na kujitolea kwake katika uongozi.
“ODM ni chama imara na thabiti, na uchaguzi wetu wa hivi karibuni katika ngazi za mashinani ulishuhudia uimara wetu kama chama chenye nguvu zaidi nchini.
"Uendelezaji wa habari za kuchochea na za kupotosha dhidi yake si tu unampotosha, bali pia unadhalilisha urithi wake na maadili anayoyasimamia,” aliongeza.
Wakati wa mazishi ya Ojwang’, familia, marafiki na viongozi kadhaa wa kisiasa walitoa heshima zao za mwisho kwa mwalimu huyo aliyeuawa, kifo chake kikiwa kimeangazia kwa mara nyingine tena ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu na vyombo vya usalama.
Viongozi wa kisiasa walikanusha madai kuwa nafasi zao serikalini zimewafanya kufumbia macho unyanyasaji wa serikali, hasa visa vya karibuni vya utekaji na mauaji.
“Nyinyi mnaozunguka nchini bila ajenda yoyote, mkijaribu kugawa nchi kwa misingi ya kikabila, mkijificha nyuma ya vijana wa kizazi cha Gen Z — hawa Gen Z wamekuwa waaminifu. Hawatakubali nyinyi kuteka harakati yao kwa maslahi yenu binafsi,” Wanga alisema.
“Sisi ni binadamu tu. Tunasimamia haki, iwe tupo serikalini au la. Msijaribu kututilia shaka — tumepigania taifa hili tangu uhuru,” aliongeza Millie Odhiambo, Mbunge wa Suba Kaskazini.