
Mwanaharakati Boniface Mwangi amemshambulia Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kutangaza kuwa atayaongoza maandamano ya Saba Saba.
Mwanaharakati huyo alisema Raila amepoteza uhalali na mamlaka ya kimaadili ya kuongoza maandamano ya umma nchini Kenya.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Julai 7, 2025, Mwangi alitambua mchango wa kihistoria wa kinara wa ODM katika harakati za kidemokrasia nchini, lakini akamtuhumu kwa kusaliti urithi huo kwa kipindi cha miongo kadhaa.
“Raila Odinga anadai kuwa baba wa Saba Saba. Hatutapingana na hilo, lakini tangu miaka ya 1980, amebadilika kutoka kuwa mkombozi hadi kuwa msaliti,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa wapiganiaji wenzake wa zamani wa Odinga — walioteswa, kufungwa, na kufukuzwa uhamishoni kwa kutetea mfumo wa vyama vingi — bado hawajalipwa fidia walizopewa na mahakama, huku serikali mfululizo zikipuuza madai hayo.
Kwa mujibu wa Mwangi, Odinga hajawahi kuipa kipaumbele haki wala fidia kwa wale walioteseka pamoja naye.
Mwangi pia alikosoa miungano ya kisiasa ya Odinga, akimtuhumu kwa kufanya mazungumzo ya kugawana madaraka na marupurupu na serikali zilezile zinazohusishwa na vifo na kutoweka kwa wafuasi wake.
“Amehangaika na kupoteza wafuasi wengi katika maandamano ya mitaani tangu miaka ya 1990, lakini hajawahi kuweka haki na fidia kwao kuwa masharti ya kujiunga na serikali za Moi, Kibaki, Uhuru, na Ruto,” alisema.
Mwangi alidai kuwa Odinga amepoteza ushawishi mitaani, na kwamba kizazi kipya cha wanaharakati jasiri na wanaotumia teknolojia, yaani Gen Z, ndicho kinachoongoza wimbi jipya la maandamano bila utegemezi kwa wanasiasa wa jadi.
Aidha, alitaja hatua ya hivi majuzi ya Chama cha ODM kumuagiza Mbunge Esther Passaris kuwasilisha mswada wa kupunguza maandamano kuwa ni ishara ya hofu ya chama hicho kuhusu harakati mpya za maandamano ambazo hakiwezi kudhibiti.
“Mzee huyo amepoteza uhalali, heshima, na udhibiti wa kuitisha maandamano, kwani Gen Zs wenye ujasiri sasa ndio wamiliki wa mitaa. ODM wameagiza Passaris kuwasilisha mswada wa kupiga marufuku maandamano kwa sababu Raila amepoteza nguvu ya majadiliano mitaani. Leo hii, Raila Odinga anakula meza moja na wanaotutekwa na kutuua,” alisema.
Haya yanajiri wakati taifa linaadhimisha kumbukumbu ya maandamano ya kitaifa ya Julai 7, 1990, yaliyolenga kushinikiza kurejeshwa kwa mfumo wa kisiasa wa vyama vingi, kinyume na utawala wa kiimla wa chama kimoja cha Rais Daniel arap Moi.
Licha ya marufuku ya serikali na kukamatwa kwa wanaharakati wakuu kama Kenneth Matiba na Charles Rubia, maelfu walikaidi amri hiyo, na kusababisha makabiliano makali na polisi ambayo yalisababisha vifo, majeruhi na kukamatwa kwa wengi.
Hatimaye, hali hiyo ilisababisha kufutwa kwa Kifungu cha 2A cha Katiba mwaka wa 1991, na kufungua njia ya mageuzi ya kidemokrasia.