logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Watu 10 Wauawa Wakati wa Maandamano ya Saba Saba ya Jumatatu

Tume hiyo imesema kuwa imebaini vifo kumi (10), majeruhi ishirini na tisa (29), visa viwili (2) vya utekaji nyara na watu thelathini na saba (37) kukamatwa katika kaunti kumi na saba (17) kufikia saa 12:30 jioni leo.

image
na Tony Mballa

Habari07 July 2025 - 19:57

Muhtasari


  • Biashara nyingi kote nchini zilibaki zimefungwa kutokana na hofu ya uporaji na uharibifu wa mali. Matukio ya uporaji yaliripotiwa katika kaunti sita (6), na ofisi ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge ya Kerugoya Central ilichomwa moto na watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu.
  • Shughuli za masomo zilikwama kote nchini huku shule na taasisi nyingi za elimu zikiwa zimefungwa. Tume ilipokea simu za dharura kutoka kwa wagonjwa waliokuwa hawana uwezo wa kufika katika vituo vya afya kutokana na kufungwa kwa barabara.

Jumla ya watu 10 wameuawa wakati wa maandamano ya Saba Saba yaliyofanyika Jumatatu, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR).

Tume hiyo imesema kuwa imebaini vifo kumi (10), majeruhi ishirini na tisa (29), visa viwili (2) vya utekaji nyara na watu thelathini na saba (37) kukamatwa katika kaunti kumi na saba (17) kufikia saa 12:30 jioni leo.

Tume hiyo ilieleza kuwa vizuizi vikubwa vya polisi viliwekwa katika barabara kuu na maeneo ya kuingia mijini, jambo ambalo lilitatiza kwa kiasi kikubwa usafiri wa watu, hasa katika jiji la Nairobi.

Vizuizi vya ziada viliripotiwa pia katika kaunti za Kiambu, Meru, Kisii, Nyeri, Nakuru na Embu.

“Raia wengi hawakuweza kufika kazini, licha ya agizo lililotolewa jana na Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, akiitaka watumishi wote wa serikali kufika kazini bila kukosa,” KNCHR ilisema.

Biashara nyingi kote nchini zilibaki zimefungwa kutokana na hofu ya uporaji na uharibifu wa mali. Matukio ya uporaji yaliripotiwa katika kaunti sita (6), na ofisi ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge ya Kerugoya Central ilichomwa moto na watu wanaoshukiwa kuwa wahalifu.

Shughuli za masomo zilikwama kote nchini huku shule na taasisi nyingi za elimu zikiwa zimefungwa. Tume ilipokea simu za dharura kutoka kwa wagonjwa waliokuwa hawana uwezo wa kufika katika vituo vya afya kutokana na kufungwa kwa barabara.

Mamia ya abiria walikwama kwenye vizuizi vya barabarani huku usafiri wa umma, ikiwemo wa anga na reli, ukitatizika pakubwa.

KNCHR imesema kuwa polisi wameendelea kupuuza agizo la Mahakama Kuu linalowataka maafisa wote wanaosimamia maandamano kuvaa sare rasmi na kuwa na vitambulisho wakati wote.

“Tume iliona maafisa wengi waliovaa kofia za kujificha nyuso, wakiwa hawajavaa sare, wakisafiri kwa magari yasiyo na alama maalum wakiwa doria katika kaunti za Nairobi, Kajiado na Nakuru.

“Pia, ilishuhudiwa uwepo wa magenge ya kihalifu yaliyojihami kwa silaha butu kama viboko, marungu, mapanga, mikuki, na pinde na mishale katika maeneo ya Nairobi, Kiambu, Kajiado na Eldoret. Katika Nairobi na Eldoret, magenge haya ya watu waliovaa kofia za kujificha nyuso yalionekana yakishirikiana na polisi,” KNCHR ilisema.

Tume hiyo pia ililaani vikali shambulizi lililotekelezwa jana na genge la wahuni waliovamia ofisi za Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), wakishambulia wafanyakazi pamoja na wananchi wasio na hatia waliokuwa wakitekeleza haki yao ya kikatiba ya kukusanyika na kujieleza.

Wanahabari waliokuwa wakiripoti tukio hilo katika ofisi za KHRC pia walinyanyaswa na kuporwa. Tume hiyo imetoa wito wa kukamatwa mara moja na kushtakiwa kwa waliopanga na kutekeleza shambulizi hilo, ambao walinaswa waziwazi kwenye picha za CCTV.

“Tume ina wasiwasi mkubwa na ongezeko la hivi karibuni la unyanyasaji na ukandamizaji dhidi ya Watetezi wa Haki za Binadamu (HRDs) wanaoshutumiwa kwa kuandaa maandamano yanayoendelea.

“Katika kipindi cha wiki moja iliyopita pekee, zaidi ya watetezi ishirini (20) halali wa haki za binadamu wamepigwa, kukamatwa, kufunguliwa mashtaka au kuitwa na polisi kuandika maelezo,” tume ilisema.

“KNCHR inaitaka Serikali kusitisha mara moja unyanyasaji dhidi ya Mashirika ya Kiraia, Watetezi wa Haki za Binadamu na kubadili harakati halali za utetezi wa haki kuwa uhalifu.

“Tume itaendelea kutekeleza jukumu lake la kikatiba la kulinda haki za kila mtu nchini Kenya.”

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved