logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Karua Amtaka Ruto Ahakikishe Uchaguzi wa Haki 2027 la Sivyo Ang'atuliwe Mapema

Karua alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwanja sawa wa kisiasa wakati wa uchaguzi.

image
na Tony Mballa

Habari08 July 2025 - 23:36

Muhtasari


  • Karua alielezea matamshi ya Ruto kuhusu mustakabali wa Kenya kuwa ni jaribio la kuchochea migawanyiko, na kuwataka wananchi kuungana kwa ajili ya mabadiliko.
  • Alielezea wasiwasi wake kuhusu uwepo wa watu waliovaa sare katika maeneo ya machafuko, akihoji iwapo wao ni maafisa halali wa usalama au wanamgambo.

Kiongozi wa chama cha People's Liberation Party (PLP), Martha Karua, amemtaka Rais William Ruto kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi wa urais wa mwaka 2027 unafanyika kwa haki.

Karua alionya kuwa Wakenya wana mamlaka ya kikatiba ya kumaliza utawala wa Ruto kabla ya muda wake kuisha, jambo lililozua mjadala kuhusu uwezekano wa kumaliza muhula wake mapema.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga cha humu nchini, Karua alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uwanja sawa wa kisiasa wakati wa uchaguzi.

“Ikiwa Ruto anataka tukutane naye kwenye debe, na abadili mienendo yake. Yeye pamoja na serikali yake haramu isiyo na mwelekeo. La sivyo, Wakenya wana uwezo wa kumaliza mkataba wako mapema,” alisema.

Kiongozi huyo wa PLP alimshtumu Ruto kwa kuwafukuza kwa makusudi makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili kuchelewesha mchakato wa uchaguzi.

“Ruto aliwafukuza kwa makusudi na kinyume cha sheria makamishna wa IEBC ambao muda wao wa kuhudumu bado ulikuwa halali ili kuchelewesha mchakato,” aliongeza.

Karua alikosoa uamuzi wa Ruto wa kujenga kanisa katika Ikulu ya Nairobi, akisema kuwa rais anaichukulia Ikulu kama mali binafsi badala ya taasisi ya umma.

Alidokeza kuwa Ruto huenda hayuko tayari kwa uchaguzi wa 2027, akitaja hatua za kiutawala zinazodhoofisha utendaji kazi wa IEBC.

“Kila kitu anachofanya (Ruto) ni cha mtu anayefikiri amenunua hati miliki ya Ikulu. Kwa nini hata ajenge kanisa pale? Nani alimwambia kuwa mtu anayefuata atakuwa na haja nacho? Huyu ni mtu anayechukulia Ikulu kama mali ya binafsi; si mtu anayejiandaa kuondoka,” alisema.

Aliukataa wazo la mazungumzo ya kitaifa, akisema lina hatari ya kuwafaidi wachache huku wengi wa Wakenya wakisahaulika.

Kiongozi huyo wa PLP alitoa wito kwa Wakenya kushikamana kupinga kile alichokiita "serikali isiyo na mwelekeo" na kulinda demokrasia ya taifa.

Karua alielezea matamshi ya Ruto kuhusu mustakabali wa Kenya kuwa ni jaribio la kuchochea migawanyiko, na kuwataka wananchi kuungana kwa ajili ya mabadiliko.

Alielezea wasiwasi wake kuhusu uwepo wa watu waliovaa sare katika maeneo ya machafuko, akihoji iwapo wao ni maafisa halali wa usalama au wanamgambo.

“Jioni ya leo napokea taarifa kwamba watu waliovaa sare ambao huenda ni maafisa wa usalama au ni sehemu ya wanamgambo wa jana wametawanywa katika miji yote ambayo kulikuwa na vurugu jana — Mwea, Ruiru, Thika, Rongai. Je, watu wataaminije kuwa hawa ni maafisa wa usalama na si wanamgambo waliokuja kuendeleza unyanyasaji?”

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved