
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) imethibitisha idadi ya vifo vilivyotokana na maandamano ya Saba Saba ya mwaka 2025, ikisema kuwa watu 31 waliuawa, 107 walijeruhiwa, na 532 walikamatwa kote nchini.
Pia, visa viwili vya kutoweka kwa watu kwa nguvu viliripotiwa, pamoja na uharibifu mkubwa wa mali ambao thamani yake haijabainika.
Katika taarifa iliyotolewa Jioni ya Jumanne, Julai 8, 2025, KNCHR ilisema inaendelea kufuatilia na kuchunguza ripoti zote na matukio yanayohusiana na maandamano ya Julai 7.
“Tunalani vikali ukiukaji wote wa haki za binadamu na tunasisitiza uwajibikaji kutoka kwa wahusika wote, wakiwemo polisi, raia na wadau wote,” tume hiyo ilisema.
Tume hiyo ilitoa rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kutakia majeruhi uponaji wa haraka.
Kwa mujibu wa KNCHR, maandamano yaliyofanyika katika kaunti mbalimbali yalijibiwa kwa ukatili na vyombo vya usalama na yaliandamana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Shirika hilo lilikariri kuwa ukiukaji wa haki, hasa unaotekelezwa kwa uwazi mbele ya dola, haupaswi kuachwa bila adhabu.
Tume pia ilieleza wasiwasi wake kuhusu uharibifu wa mali na ukandamizaji unaoendelea dhidi ya waandamanaji, watetezi wa haki za binadamu, na wanahabari.
Taarifa hii ya hivi punde inajengwa juu ya mkutano wa awali na wanahabari uliofanyika Jumatatu, Julai 7, 2025, ambapo KNCHR iliripoti vifo 10, majeruhi 29, utekaji wawili, na watu 37 waliokamatwa katika kaunti 17.
Wakati huo, tume pia ilionya kuhusu kufungwa kwa biashara na shule kwa wingi, uporaji katika kaunti sita, na kuchomwa kwa ofisi ya Hazina ya Maendeleo ya Maeneobunge (CDF) ya Kerugoya Central.
Aidha, huduma za afya ziliathiriwa pakubwa, huku wagonjwa wakishindwa kufika hospitalini kutokana na vizuizi barabarani. Usafiri wa umma, ikiwemo reli na anga, ulisimama kabisa.
KNCHR pia ilikosoa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa kukaidi agizo la Mahakama Kuu linalowataka maafisa wa polisi kuvaa sare rasmi na kujitambulisha wakati wa maandamano. Katika maeneo mengine, iliripotiwa kuwa magenge ya wahalifu yalikuwa yakishirikiana na polisi.
Tume hiyo imetaka kufanyika kwa uchunguzi wa haraka na uwajibikaji, ikisisitiza haki ya Wakenya ya kukusanyika kwa amani chini ya Kifungu cha 37 cha Katiba.