
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua aliondoka nchini usiku wa Jumatano kuelekea Marekani.
Akizungumza na wanahabari mapema siku hiyo, Gachagua alisema ziara yake inalenga kuzungumza na Wakenya waishio ughaibuni pamoja na wadau wa kimataifa.
Safari hiyo ndiyo ya kwanza kwa Gachagua kusafiri nje ya nchi tangu aondolewe madarakani mwezi Oktoba 2024.
"Usiku wa leo nitasafiri kuelekea Marekani kuzungumza na Wakenya waishio ughaibuni na jamii ya kimataifa kuhusu hali ya taifa," alisema katika mkutano na wanahabari uliofanyika mapema siku hiyo.
Aliondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta akiagwa na mkewe, Mchungaji Dorcas Rigathi, pamoja na wandani wake kadhaa akiwemo Seneta wa Nyandarua John Methu, Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Jane Njeri Maina, aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, na viongozi wengine.
Gachagua, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), alifichua mwezi uliopita kuwa angefanya ziara ya miezi miwili nchini Marekani.
Anatarajiwa kutembelea maeneo ya Dallas, California, Seattle, Boston na Baltimore, ambako atafanya mikutano ya hadhara (town hall meetings) na kushiriki mikusanyiko ya kijamii ili kueneza ajenda yake kwa jamii ya Wakenya ughaibuni.
Ingawa bado hajatangaza rasmi kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, Gachagua ameapa kuendeleza juhudi za kuhakikisha Rais William Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee.
Chini ya kaulimbiu ya 'wantam', yeye pamoja na viongozi wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa People’s Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i wameanzisha kampeni kali ya uhamasishaji kuelekea uchaguzi ujao.
Vyanzo vinaeleza kuwa Gachagua pia amepanga kukutana na wawekezaji kutoka Marekani wanaoripotiwa kuwa na nia ya kushirikiana na upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027.
Ziara yake inajiri siku chache tu baada ya Matiang’i kuanza kampeni yake ya kuwania urais 2027 katika uwanja wa kimataifa, kwa kuanza mikutano ya Wakenya wa diaspora kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika Texas.