
Mbunge wa Imenti Kaskazini, Rahim Dawood, amekishutumu chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Rigathi Gachagua kwa kupanga vurugu zilizotokea Meru wakati wa maadhimisho ya Saba Saba.
Mbunge huyo alidai kuwa chama hicho kipya cha kisiasa kilihusika katika kuwasafirisha wahuni walioshiriki maandamano ya Saba Saba mjini Meru.
Akizungumza na wanahabari Jumatano, Julai 9, wakati jumuiya ya wafanyabiashara wa Meru iliwasilisha ombi lao kwa afisi ya kamishna wa kaunti, Dawood alidai kuwa maafisa wa chama hicho waliandaa vurugu hizo kwa hasira.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya maafisa wa DCP, ambao hakuwataja kwa majina, walikasirishwa na sifa ambazo Rais William Ruto na naibu wake Kithure Kindiki walipokea walipotembelea kaunti hiyo hivi majuzi katika hafla ya Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Wakulima wa Maziwa.
“Wiki chache zilizopita, rais na naibu wake walihudhuria hafla hapa ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Meru Dairy, Kenneth Gitonga, alilisifia serikali kwa usaidizi wake. Maafisa wa DCP waliapa kufundisha kampuni hiyo adabu,” alidai Dawood.
Mbunge huyo alilaani vikali uharibifu uliofanyika kaunti ya Meru na kusema kuwa hali hiyo haikubaliki.
Wakati wa maandamano hayo, Supermarket ya Magunas ilichomwa moto, huku maduka mengine yakiporwa na wahuni.
“Hili si jambo la kawaida. Mwaka huu hatukuwa na maandamano kuhusu Mswada wa Fedha, na nasema haya kwa uhakika — yote haya yaliandaliwa na chama cha DCP,” alisema.
Kufuatia uharibifu huo, mbunge huyo alisema kuwa wafanyabiashara na wakazi hawataruhusu tukio kama hilo kujirudia tena siku za usoni.
Aliwataka wafanyabiashara wa Meru kuiga mfano wa jumuiya ya wafanyabiashara wa Nairobi kwa kulinda biashara zao.
Alisisitiza kuwa hawapaswi kuogopa kulinda chanzo chao cha mapato.
“Watu wakiwaita wahuni ilhali mnalinda mali yetu, msijali,” aliwaambia wafanyabiashara hao. Wafanyabiashara wa Meru waliwasilisha ombi kwa kamishna wa kaunti wakitaka kulindwa kwa biashara na mali zao.
Pia aliwataka wanafunzi kutoka taasisi mbalimbali za elimu ndani ya Kaunti ya Meru kuepuka kushiriki maandamano, akiwasihi wasikubali kutumiwa na wanasiasa.
Kaunti hiyo ina taasisi kama Meru National Polytechnic, Chuo Kikuu cha Meru, pamoja na vyuo vingine vya kati.
“Msikubali kutumiwa na wanasiasa. Mkikamatwa, tutawasilisha majina yenu kwa Wizara ya Elimu ili msiweze kusoma popote pengine,” Dawood alionya.
Aidha, alizitaka idara za usalama zichukue hatua madhubuti na kuhakikisha wote waliohusika na maandamano ya vurugu na uharibifu wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria ili haki itendeke kwa walioathirika.