
Rais William Ruto amewaambia maafisa wa polisi kuwapiga risasi miguuni watu wanaokamatwa wakivamia biashara na kuharibu mali wakati wa maandamano.
Akizungumza Jumatano wakati wa uzinduzi wa mradi wa makazi ya polisi katika eneo la Kilimani, Nairobi, Rais aliwaeleza maafisa wasiwaue waandamanaji, bali "wapige risasi na wavunje miguu" ya yeyote mwenye fujo.
“Mtu yeyote anayechoma biashara au mali ya mwingine, apigwe risasi mguuni, aende hospitali kisha mahakamani. Ndiyo, wasiwaue, lakini wapigwe na miguu ivunjike. Kuharibu mali ya watu si sawa,” alisema.
Ruto aliwaonya viongozi wa kisiasa ambao hakuwataja moja kwa moja, akiwatuhumu kwa kuchochea vijana kufanya fujo.
“Ni viongozi wanaofadhili vijana kutekeleza vitendo hivyo, na tunawafuata!”
Alisema mashambulizi dhidi ya polisi na vituo vyao, kama vile yalivyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kumbukumbu ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 mnamo Juni 25, yatachukuliwa kama ugaidi.
“Wanaovamia polisi wetu, vituo vya usalama vikiwemo vituo vya polisi, wanatangaza vita. Huo ni ugaidi, na tutashughulika nanyi kwa ukali. Hatuwezi kuwa na taifa linaloendeshwa kwa hofu na vurugu. Haitatokea nikiwa madarakani,” alisema Ruto.
Maandamano yameongezeka kote nchini Kenya katika miezi ya hivi karibuni kufuatia malalamiko dhidi ya utawala wa Ruto kuhusu gharama ya juu ya maisha na msako dhidi ya wakosoaji wa serikali na maandamano ya mitaani, mengi yakiwa yamesababisha vifo, majeraha na utekaji.
Wakosoaji wameilaumu polisi kwa ukatili na kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji wasio na silaha wakati wa maandamano yanayoongozwa na vijana.
Wakati huo huo, kumekuwa na hofu kuhusu kuhusishwa kwa ‘goons’ — makundi ya vijana waliokuwa na marungu na viboko waliotumiwa kushambulia waandamanaji na kupora biashara.
Katika maandamano ya karibuni zaidi ya Jumatatu, Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) iliripoti vifo 31 na majeruhi 107.
Matukio ya uharibifu wa mali ya biashara pia yaliripotiwa katika miji kadhaa katika angalau kaunti 15.
Maandamano ya Juni 25 yalipelekea zaidi ya watu 16 kuuawa, wengi wao kwa mikono ya polisi, kwa mujibu wa shirika la Amnesty International Kenya.
Mbali na biashara, makundi ya vijana pia yalivamia angalau vituo tisa vya polisi, na kuchoma angalau vitano, pamoja na mahakama na ofisi za serikali ya kaunti na magari yake.
Agizo la Ruto la Jumatano linakuja baada ya matamshi tata ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kufuatia vurugu za maandamano ya Juni 25, ambapo aliwaambia polisi wawaue wote wanaokaribia vituo vya polisi.
Waziri huyo aliwaambia polisi: “Mtu yeyote anayekaribia kituo cha polisi, mpige risasi. Mbona mtu anayekuja kuiba bunduki aachwe? Bunduki si donuts!”