
Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, amepuuzilia mbali uwezekano wa kuwasilisha hoja ya kumng’oa Rais William Ruto madarakani.
Kupitia akaunti yake rasmi ya X, Mbunge huyo alijibu Mkenya mmoja aliyekuwa akimkosoa kwa kushiriki maandamano dhidi ya Ruto huku akiwa na uwezo wa kuanzisha mchakato wa kumuondoa madarakani akiwa bungeni.
“Mara nyingi humuona Babu Owino akiwa kwenye maandamano, jambo linalonifanya niulize, kama kweli anataka Ruto aondoke, kwa nini basi hasisababishe hoja ya kumng’oa bungeni?” aliuliza Mkenya huyo kwenye X.
Katika jibu la haraka, Babu Owino alijitetea kwa kutowasilisha hoja hiyo, akisema asilimia 90 ya wabunge tayari wamekwisha pewa hongo au kushawishiwa, na hivyo hoja hiyo haitafaulu.
“Baba yako ataunga mkono hiyo hoja bungeni? Mimi sijui kushindwa kwa sababu asilimia 90 ya wabunge wameshawishika,” Babu Owino alijibu.
Wito wa kumng’oa Rais Ruto ulizuka baada ya kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua, kuwataka wabunge waanzishe mchakato huo.
Alidai kuwa hatua hiyo “itatoa nafasi ya kueneza ujumbe na kuwaamsha Wakenya pamoja na dunia kuhusu kile kinachoendelea.”
“Bunge linaweza kujikomboa, na hata wale wachache wanaosema ukweli kwa niaba ya wananchi wanaweza kuanzisha hoja ya kumuondoa rais,” alisema Karua.
Mbunge anaruhusiwa kuanzisha hoja ya kumng’oa rais iwapo kuna ukiukaji mkubwa wa Katiba au sheria nyingine yoyote. Hoja hiyo lazima iungwe mkono na angalau theluthi moja ya wabunge wote.
Mnamo mwaka wa 2015, wabunge wa upinzani waliibua gumzo baada ya takriban wabunge 105 kusaini hoja ya kumng’oa aliyekuwa Rais wakati huo, Uhuru Kenyatta, wakidai alikuwa amekiuka Katiba.
Babu Owino Alaani Ukatili wa Polisi Siku ya Saba Saba
Hata hivyo, hoja hiyo haikufua dafu, na hivyo hakuna rais ambaye amewahi kuondolewa madarakani kupitia bunge.
Mbunge wa Embakasi Mashariki ni miongoni mwa wanasiasa wachache wanaojiunga na vijana wa Kenya wakati wa maandamano yao.
Wakati wa maandamano ya kumbukumbu ya Juni 25, Babu Owino alijiunga na vijana wa kizazi cha Gen Z katikati mwa jiji la Nairobi, ambako alipokelewa kwa furaha na shangwe kubwa.
Owino pia amekuwa mstari wa mbele kutetea uongozi bora, akilaani visa vya ukatili wa polisi ambavyo vimekuwa vikiongezeka nchini.