
Naibu Rais Kithure Kindiki ameonya wanasiasa dhidi ya kujaribu kuingia mamlakani kwa kutumia vurugu au njia zisizo halali.
Akizungumza Alhamisi wakati wa mpango wa kuwawezesha wanawake katika Kaunti ya Trans Nzoia, Kindiki alisisitiza kuwa uongozi utaamuliwa tu kupitia uchaguzi unaosimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
“Hatutaruhusu wanasiasa wenye tamaa ya madaraka kutumbukiza nchi yetu katika machafuko na vurugu. Wale wanaotafuta njia za mkato kuingia uongozini wanapaswa kutulia,” alisema.
“Tarehe ya uchaguzi inajulikana, na IEBC sasa iko ofisini. Wangoje.”
Kindiki aliongeza kuwa hakuna mtu atakayekubaliwa kuchochea vurugu, kuvamia taasisi za serikali au kuharibu mali ya umma au binafsi kwa nia ya kutwaa mamlaka kwa nguvu.
“Hakuna mtu tutaruhusu avamie kituo cha polisi, aingie Ikulu kwa nguvu ama achochee uharibifu wa mali ya umma na ya kibinafsi ili aingie uongozini kwa lazima kupitia shortcut,” alisema Kindiki.
Naibu Rais alibainisha kuwa kurejea kwa makamishna wa IEBC baada ya mivutano ya kisheria kunafungua njia ya maandalizi sahihi ya uchaguzi.
“Kwa muda, hatukuwa na IEBC kutokana na migogoro mahakamani. Sasa mahakama imetatua masuala hayo na makamishna wako ofisini. IEBC ndiye mwamuzi. Wajibu wa kuandaa uchaguzi uko mikononi mwa IEBC,” alisema.
Kindiki alisisitiza kuwa Katiba iko wazi kuhusu majukumu ya IEBC na kwamba serikali inaheshimu taasisi zote huru.
Aidha, aliwakosoa wanasiasa wanaosubiri vipindi vya kampeni kugawa bidhaa za bei rahisi kama vile reflecta na leso, akisema kuwa uongozi wa kweli unajitokeza kupitia juhudi madhubuti za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“Huu ndio wakati wa kusimama na wananchi kupitia shughuli madhubuti za kuwawezesha kiuchumi,” alisema Kindiki.
“Wale wanaosubiri kampeni ili watoe vitu vya bei rahisi wanaonyesha dharau kwa wapiga kura.”