logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Salasya Amkemea Vikali Natembeya kwa Kudai Jamii ya Waluhya ni 'Watchmen' na 'Maids'

Alisisitiza heshima na bidii ya jamii hiyo, akibainisha kuwa Waluhya wanahudumu katika sekta mbalimbali zenye umuhimu mkubwa.

image
na Tony Mballa

Habari11 July 2025 - 09:29

Muhtasari


  • Salasya alitaja matamshi ya Natembeya kuwa ni dhihaka ya kitabaka, akisisitiza kuwa heshima kwa kila aina ya kazi ni msingi wa uongozi wa kweli.
  • Salasya alihimiza mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wa kila asili, akiwaonya wasikubali kudharauliwa na wanasiasa.

Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, amemshambulia vikali Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, kwa kudai kuwa watu wa jamii ya Waluhya hupata kazi duni pekee kama vile wasaidizi wa nyumbani na walinzi.

Salasya alipinga vikali kauli hiyo ya Natembeya, akisema inadharau mchango mkubwa wa jamii ya Waluhya katika jamii.

Alisisitiza heshima na bidii ya jamii hiyo, akibainisha kuwa Waluhya wanahudumu katika sekta mbalimbali zenye umuhimu mkubwa.

“Aibu kwa Natembeya! Unawezaje, George Natembeya, kufungua mdomo wako na kuidhalilisha jamii ya Waluhya, jamii ya watu wenye kujivunia kazi na bidii, kwa kuwashusha hadhi kuwa wasaidizi wa nyumbani, walinzi na mafundi? Ni nani alikupa ujasiri wa kuwakejeli watu wanaojenga taifa hili kwa jasho, heshima, na maadili ya kazi yasiyo na kifani?” aliuliza Salasya.

“Ni wazi unazama katika kiburi kiasi cha kusahau kwamba hao Waluhya unaowadhihaki ndio wanaolinda malango yako, kusafisha ofisi zako, kujenga nyumba zako, na kulinda familia zako kwa uaminifu na unyenyekevu. Kama ungelilea kwa maadili mema, ungalijua kuwa kuna heshima katika kila kazi – lakini ulimi wako wa mabwanyenye umebainisha ufisadi wa tabia zako,” aliongeza.

Salasya alitaja matamshi ya Natembeya kuwa ni dhihaka ya kitabaka, akisisitiza kuwa heshima kwa kila aina ya kazi ni msingi wa uongozi wa kweli.

“Hili si tusi la kikabila pekee, ni dharau ya kitabaka. Mtu asiyeweza kuheshimu kazi halali hana sababu ya kujifanya kiongozi! Huwatukani watu kwa kazi wanazofanya. Unawashukuru. Unawawezesha. Unawatia moyo.”

Alieleza kuwa jamii ya Waluhya hujivunia kazi yao, na hawapaswi kuona aibu kwa kazi wanazofanya.

“Ijulikane wazi: Waluhya hawana aibu ya kufanya kazi. Tunajivunia jasho letu. Tunajenga, tunahudumu, tunaongoza – kwa mikono na mioyo yetu. Na hatutakubali kutishwa wala kudhalilishwa na ndimi za kisiasa za bei rahisi zinazotafuta makofi kwenye kumbi zisizo na watu.”

Salasya alihimiza mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wa kila asili, akiwaonya wasikubali kudharauliwa na wanasiasa.

“Kwa kila mlinzi, kila msaidizi wa nyumbani, kila mfanyakazi wa mjengo – awe Mluhya au la – ninyi ndiyo uti wa mgongo wa taifa hili. Msikubali mwoga aliyevaa suti kuwavunjia heshima. Tunainuka kwa kuinua wengine, si kwa kuwakejeli.”

“Mhe. Peter Kalerwa Salasya anasimama imara – bila kutetereka, bila kununuliwa, bila kuinama – kukumbusha: ukiwadhalilisha watu wetu tena, tutakukabili kwa ukweli, moto na upinzani.”

Hata hivyo, katika majibu yake, Gavana Natembeya alimkosoa Salasya kwa kumwita “mtoto mdogo” na kutetea kauli zake kuwa ni uhalisia wa hali ya maisha ya jamii ya Waluhya nchini.

“Salasya ni mtoto mdogo ambaye hakuwepo wakati Katibu Mkuu wa zamani wa KANU, Joseph Kamotho, alipowaita Waluhya walinzi na wasaidizi wa nyumbani. Mtazamo wake ulikuwa wa kweli kabisa.

“Wakenya wanajua jambo hili ni ukweli. Unaangalia tu yule msichana anayekufanyia kazi ametoka wapi; yule jamaa ambaye anayelinda boma lako ametoka wapi. Na mara nyingi nawaambia Wakenya waende waulize yule jamaa ambaye ameshika rungu kwa gate amesoma hadi wapi. Utapata kuwa amefuzu kutoka chuo kikuu lakini hajapata fursa ya kupata kazi aliyosomea.

“Ni jinsi mambo yanavyoendeshwa nchini. Kama hauna mtu mwenye ushawishi serikalini, mambo yako hayaendi vizuri,” alisema Natembeya.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved