
Ida Odinga, mke wa kiongozi wa ODM Raila Odinga, ametoa wito wa dhati kwa vijana wa Kenya kujiepusha na maandamano yanayoendelea kupinga serikali.
Akizungumza Ijumaa, Julai 11, huko Migori wakati wa mazishi ya mtoto wa Mbunge wa Suna West, Peter Masara, Ida alieleza kusikitishwa kwake na idadi inayoongezeka ya vifo vya vijana vinavyotokana na maandamano ya hivi majuzi.
Aliwahimiza vijana kufikiria mateso ambayo familia zao hupitia wanapopoteza wapendwa wao katika makabiliano hayo.
“Kabla hujatoka kwenda kuandamana, fikiria umetoka wapi. Ukifa huko, mama yako – na mimi – tunabaki na huzuni. Nawaomba, tafadhali msitoke,” alisema.
Ida pia alilaani ukatili wa polisi, akiwatuhumu maafisa wa usalama kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya vijana wasio na silaha.
Akizungumza kwa msisitizo akitumia mfano wa Biblia, aliufananisha uchungu wa kina mama wanaowazika watoto wao na simulizi ya Raheli aliyekuwa akilia kwa ajili ya wanawe.
“Tunasoma Biblia na tunaona Raheli alihuzunika sana watoto wa kiume walipokuwa wakiuawa.
“Vivyo hivyo, mimi pia sifurahishwi hata kidogo na mauaji na ulemavu unaowapata vijana wetu. Haijalishi ni wapi, ni makosa kwa kila hali, na nimekasirika sana,” alisema Ida.
Ida, ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Canon katika Kanisa la Anglikana la Kenya, pia aliwakemea vikali vijana waliomhangaisha na kumkabili gavana wa ODM waliyehudhuria mazishi hayo, akitaja tabia hiyo kuwa “isiyo na staha” na kukosa heshima.
“Nilikasirishwa sana na tabia yenu mbaya. Haiwezekani kumsukuma gavana namna hiyo.”
“Tuko hapa kuomboleza, hatuko hapa kufanya siasa. Tabia hiyo ni ya kihuni na haifai kurudiwa,” Ida alisema.
Kauli zake zinajiri wakati Kenya ikishuhudia wimbi la maandamano yanayoongozwa na vijana, yakiendeshwa na hali ngumu ya kiuchumi na madai ya ukatili wa polisi.
Kwa mujibu wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), zaidi ya vijana 30 waliuawa wakati wa maandamano ya Saba Saba pekee.