logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wamalwa: Gen Z Hawawezi Kumng’oa Ruto Madarakani Bila Usaidizi wa Wanasiasa Wazoefu

Wamalwa aliwasihi vijana watambue kwamba kuibadilisha nchi kutahitaji ushirikiano na raia wengine.

image
na Tony Mballa

Habari15 July 2025 - 14:13

Muhtasari


  • Akizungumza Jumatatu katika mahojiano na runinga ya TV47, Wamalwa alipendekeza kuwa vijana lazima washirikiane na viongozi wa kisiasa waliobobea ili kuleta mabadiliko ya kisiasa yenye maana.
  • Aliifananisha harakati za sasa zinazoongozwa na Gen Z na juhudi za kisiasa za kundi la "Young Turks" katika miaka ya 1990, akibainisha kuwa walifaulu tu baada ya kushirikiana na wanasiasa waliokuwepo kwa muda mrefu.

Kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), Eugene Wamalwa, amesema kuwa kizazi cha Gen Z hakiwezi kumng’oa Rais William Ruto madarakani kupitia maandamano pekee.

Akizungumza Jumatatu katika mahojiano na runinga ya TV47, Wamalwa alipendekeza kuwa vijana lazima washirikiane na viongozi wa kisiasa waliobobea ili kuleta mabadiliko ya kisiasa yenye maana.

Aliifananisha harakati za sasa zinazoongozwa na Gen Z na juhudi za kisiasa za kundi la "Young Turks" katika miaka ya 1990, akibainisha kuwa walifaulu tu baada ya kushirikiana na wanasiasa waliokuwepo kwa muda mrefu.

“Kumtoa Rais Ruto ni lazima tukumbuke kuwa aliwahi kuwa mwanafunzi wa Daniel Arap Moi; ni sawa na kujaribu kumtoa Moi,” alisema Wamalwa.

“Wakati Young Turks walijaribu kumwondoa Moi peke yao, hawakufaulu. Ni baada tu ya kuchukua mkondo wa kushirikiana kwa wote, kwa kuwaleta viongozi kama Jaramogi Oginga Odinga, Kenneth Matiba, Charles Rubia na Mwai Kibaki, ndipo walipofanikiwa.”

“Wanasema kidole kimoja hakivunji chawa. Ni Young Turks walioshirikiana na wazee, yaani wanasiasa wenye uzoefu, ndipo jambo hilo likawezekana. Haitakuwa maandamano ya Gen Z pekee, japo walikuwa karibu. Itahitaji mbinu ya ‘Gen Zote’ — ushirikiano wa kila mtu — kuleta mabadiliko ya kisiasa.”

Wamalwa aliwasihi vijana watambue kwamba kuibadilisha nchi kutahitaji ushirikiano na raia wengine, wakiwemo wale walio na uzoefu wa uongozi.

Eugene Wamalwa

“Kuna jambo lazima niwaambie Gen Z wanaosema hawataki wazee waliowahi kuwa serikalini — kwamba uzoefu hauna maana,” alisema.

“James Madison alisema kwamba kama tungekuwa taifa la malaika, tusingehitaji serikali. Msitegemee malaika kushuka kutoka mbinguni kuja kubadilisha nchi yetu. Ni Wakenya wa kawaida, waliozaliwa na kulelewa hapa, ambao rekodi na uwezo wao ndivyo vitakavyofanya tofauti.”

Waziri huyo wa zamani alisisitiza pia umuhimu wa uadilifu na huruma katika uongozi, akisema kuwa Wakenya kwa sasa wanajali zaidi nani hafai kurejea madarakani kuliko nani anafaa kuwa rais ajaye.

“Kilicho muhimu zaidi si nani kati yetu atakayekuwa rais ajaye, bali ni nani hafai kuwa rais wa Kenya tena,” alisema Wamalwa.

“Hili si suala la kupindua serikali. Ni kuhakikisha kwamba baada ya muhula mmoja, Wakenya wanachagua viongozi wenye uadilifu na huruma, viongozi wanaoheshimu maisha na mali ya watu.”

Aliongeza kuwa Wakenya watakuwa wakitafuta kiongozi atakayeweza kuunganisha nchi na kushughulikia changamoto zinazowaumiza raia, kama vile kupanda kwa bei ya mafuta.

“Uadilifu utakuwa kwenye debe. Wakenya watataka rais mwenye rekodi safi, atakayebadilisha nchi hii na kupitia upya sera ambazo zimefeli,” alisema.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved