
Aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga amefichua kuwa kampeni yake ya kuwania urais mwaka wa 2027 itagharamiwa kwa kiasi kikubwa kupitia michango ya wananchi.
Maraga alieleza mkakati wake wa kugharamia kampeni hiyo wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha televisheni cha humu nchini mnamo Julai 15, 2025.
Alisema anatarajia kuchangia kati ya shilingi milioni moja hadi mbili kutoka kwa mali yake binafsi, huku akitegemea Wakenya kuchangia kiasi kilichosalia.
“Kidogo sana. Yaani, shilingi milioni moja au mbili. Sina pesa nyingi,” alikiri alipoulizwa kuhusu mchango wake binafsi kwa kampeni hiyo.
“Tutaomba Wakenya wafadhili kampeni yetu, na kampeni hii itafaulu. Wananchi wenyewe wataigharamia uchaguzi huu,” Maraga alisisitiza.
Jaji Mkuu huyo wa zamani alisema kuwa kampeni inayofadhiliwa na wananchi itasaidia kulinda uhuru dhidi ya ushawishi wa nje, akiitaja kama “urais wa Wanjiku” usioongozwa na maslahi binafsi.
“Mara tu tukifadhiliwa na kuchaguliwa, yeyote atakayejaribu kutuingilia au kutulazimisha atambue kuwa huu ni urais wa Wanjiku,” alisema.
Alipoulizwa iwapo mpango wa kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi ni wa kweli ikizingatiwa hali ngumu ya kiuchumi inayoikumba nchi, Maraga alieleza kuwa anaamini kampeni hiyo itapata uungwaji mkono kutoka kote nchini, hata kwa michango midogo.
“Hatutaki pesa nyingi kutoka kwa mtu mmoja. Kwa mateso ambayo Wakenya wamepitia, naweza kukuahidi kuwa tutapata michango ya shilingi 10, 20, 50 kutoka kwa mtu mmoja—hata mia moja,” alisema.
Maraga alibainisha kuwa mazungumzo ya awali na wafuasi wake yamekuwa ya kutia moyo, baadhi yao tayari wakiulizia mbinu za kutoa michango.
“Watu tunaowazungumzia, wale tunaokutana nao, wanasema, tuambie tu ni lini mnapanga kuweka paybill. Tuko tayari kuchangia,” Maraga alieleza.
Alionesha imani kubwa katika mfumo huo wa ufadhili, hata akitabiri uwezekano wa kuwa na ziada ambayo itatumika kwa shughuli za kijamii.
“Kusema kweli, tunatarajia kuwa na ziada. Na kwa mtazamo wangu, tukipata ziada, kiasi hicho kitapelekwa kwenye miradi ya manufaa ya umma,” alisema.
Aidha, aliahidi kuweka wazi bajeti ya kampeni hiyo pamoja na maelezo ya ufadhili kwa wakati ufaao.