
Mbunge wa Lang’ata, Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o, ameonyesha imani thabiti kuwa Rais William Ruto atapata muhula wa pili katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2027.
Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na mtangazaji wa vyombo vya habari Alex Mwakideu mnamo Alhamisi, Julai 17, 2025, Jalang’o alisema kuwa inazidi kuwa vigumu kumng’oa Ruto madarakani.
Alisisitiza kuwa Ruto yuko katika mkondo wa kurejea Ikulu na anaelekea kushinda kwa tofauti kubwa.
Kwa mujibu wa Jalang’o, hakuna mgombea wa urais mwenye nguvu wa kuweza kumshinda Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
“Ruto kurudi inaenda kuwa ngumu na kumtoa ndio inaenda kuwa ngumu zaidi, Rais William Ruto ndio anaenda kuwa rais tena, anaenda kushinda mbali sana. Sijaona mtu anaweza kumtoa,” alisema Jalang’o.
“Sijaona mtu wa kumtoa ama kumsumbua ndio sababu unaona anaongea akiwa na ile confidence anasema ‘sahi siasa bado itafika itaamuliwa.’”
Mbunge huyo mchanga alikiri kuwa kuna presha halisi kutoka kwa wananchi pamoja na presha ya kisiasa inayomkabili Rais.
Alisema kuwa tayari kuna watu wengi ambao wameridhika na kazi ambayo Ruto ameifanya hadi sasa, japo mvutano wa kisiasa bado upo.
Ijapokuwa serikali ya Ruto imetimiza miaka miwili na nusu madarakani, Jalang’o alibainisha kuwa ahadi nyingi zilizotolewa wakati wa kampeni ndio zinaanza kutekelezwa au bado hazijakamilika.
Aliongeza kuwa ni suala la muda tu kabla ya wananchi kutambua kazi iliyofanyika, kwani matokeo yataanza kuonekana.
“Hiyo pressure kuna ya ukweli ya watu ambayo hawajaridhika na mheshimiwa Rais na utendakazi wake na pia kuna pressure ya kisiasa. Na kama ni utendakazi wake, amekuwa miaka miwili na nusu lakini kuna mambo mengi aliyoyaahidi na zimeanza kutimia, na muda si mrefu watu wataanza kuappreciate kuwa kazi ilikuwa ikifanyika, he will be able to show something,” aliongeza.
Kauli hizi zinajiri baada ya Rais Ruto kutangaza kuwa atashinda uchaguzi mkuu wa 2027 kwa kishindo dhidi ya upinzani, licha ya muungano wa upinzani unaoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuapa kumng’oa mamlakani.
Akizungumza katika mji wa Kisumu kabla ya uzinduzi wa mradi wa makazi ya bei nafuu wa LV Point katika LV Marina mnamo Alhamisi, Mei 29, 2025, Ruto alisema kuwa upinzani hauna mpango wala ajenda kwa wananchi wa Kenya.
“Hawa ni watu wasio na maono, wasio na mpango, na wasio na ajenda. Tutawaonyesha vumbi, hawataamini,” alisema.
“Wanaojua tu ni kauli mbiu: ‘Ruto must go,’ ‘Kasongo,’ ‘Wantam…’ Na nataka kuwaambia kuwa tutaendelea kupeleka nchi hii mbele.”