
UASIN GISHU, KENYA, Julai 24, 2025 — Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, amemkemea vikali Katibu Mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna, kwa madai ya kutaka shilingi milioni 300 ili kujiunga na serikali ya Rais William Ruto.
Sudi alitoa matamshi hayo, alipohutubu katika mazishi ya Richard Kiprotich Kirorei katika kijiji cha Cheukta, eneobunge la Soy, Kaunti ya Uasin Gishu.
“Mahitaji ya Sifuna ya shilingi milioni 300 ili awe sehemu ya serikali jumuishi ni ya kushangaza; ni wazi kuwa anawaza kujinufaisha badala ya kuhudumia wananchi,” alisema Sudi.
Aliendelea kumshambulia Sifuna kwa kile alichokitaja kuwa siasa za ulafi na masharti ya kifedha.
“Aendelee kupiga kelele kadri atakavyo, lakini sisi hatumpi hata senti. Afadhali tutumie hizo fedha kujenga barabara kijijini kwao,” aliongeza.
Sudi pia alisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza haitakubali kushurutishwa kwa misingi ya tamaa ya kisiasa.
“Serikali hii si ya kuhongwa. Hatutakuwa na mazungumzo ya pesa. Tuko tayari kushirikiana na watu wa nia njema, si wenye tamaa,” alisema.
Aliwashutumu pia viongozi wanaopinga ushirikiano kati ya Raila Odinga na Rais Ruto kuwa wanafiki wanaotafuta manufaa binafsi.
“Wamekuwa wakililia mazungumzo ya kitaifa, sasa yanapokuja wanataka mabilioni. Huo si uongozi bali ni biashara ya kisiasa,” alisema Sudi.
Sudi aliandamana na viongozi wengine akiwemo Mbunge wa Soy David Kiplagat, Naibu Spika wa Uasin Gishu Sarah Malel, Mwakilishi wa Wanawake wa Taita Taveta Haika Lydia Mizighi, Katibu wa Habari wa PSC Emmanuel Tallam, MCA wa Nakuru George Kanure, pamoja na madiwani na viongozi wa mitaa.