
MIGORI, KENYA, Julai 27, 2025 — Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya, Kithure Kindiki, ametambuliwa rasmi kama mzee wa jamii ya Waluo katika hafla maalum iliyofanyika Ong’er Grounds, Nyatike – hatua inayochukuliwa kama ishara ya mshikamano wa kitaifa na heshima kwa tamaduni za makabila mbalimbali.
Katika tukio lililojaa shamrashamra za kitamaduni, Naibu Rais Kithure Kindiki alivalishwa mavazi rasmi ya uongozi wa kijadi wa jamii ya Waluo na kukabidhiwa mkuki na ngao kama ishara ya ulinzi kwa taifa.
Akitunukiwa jina la "Odhiambo", viongozi wa jamii walieleza kuwa jina hilo linawakilisha mtu mwenye tabia ya amani, utulivu na hekima, sifa ambazo Kindiki amejulikana nazo.
“Ninapokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Inaashiria mshikamano wa kitaifa na mapenzi ya kweli kwa mila na tamaduni za watu wetu,” alisema Naibu Rais baada ya kutawazwa.
Katika hafla hiyo ya uwezeshaji wa kiuchumi, Kindiki alieleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kaunti ya Migori na maeneo jirani, ikiwemo barabara, huduma za afya, na uwezeshaji wa vijana na wanawake.
“Lazima tuwe viongozi wa mfano. Mzee Raila Odinga ametufunza kuweka taifa mbele ya maslahi binafsi,” alisema Kindiki, akimpongeza kiongozi huyo wa upinzani kwa mchango wake katika mshikamano wa kitaifa.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Waziri wa Fedha John Mbadi, Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, Gavana wa Migori Ochillo Ayacko, Mwakilishi wa Wanawake Migori Fatuma Mohamed, Mbunge wa Nyatike Tom Odege, Seneta Eddy Oketch, na msaidizi binafsi wa Rais Farouk Kibet.
Hafla hiyo imefanyika miezi michache tu baada ya Rais William Ruto na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kutawazwa pia kuwa wazee wa jamii ya Waluo wakati wa tamasha la Piny Luo Festival lililofanyika Siaya mwezi Januari, likiongozwa na Raila Odinga.