
NAIROBI, KENYA, Julai 29, 2025 — Kamati Kuu ya Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ikiongozwa na Kiongozi wa Chama Raila Odinga, imekutana leo Nairobi na kupitisha maazimio saba muhimu yanayobadilisha kabisa dira ya chama hicho.
Katika taarifa yao rasmi, chama hicho kilitangaza kuwa kitaunga mkono ushirikiano na serikali ya Kenya Kwanza kupitia utekelezaji wa Mkataba wa Maelewano (MOU) uliotiwa saini na kuhakikisha kuwa masilahi ya wananchi yanawekwa mbele.
"Tunaunga mkono msimamo wa Kiongozi wa Chama, Mheshimiwa Raila Odinga, wa kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza ili kustahimili misukosuko ya taifa letu kupitia njia za kikatiba na kidemokrasia," ilisomeka sehemu ya taarifa ya Kamati Kuu.
ODM ilitangaza kuunda kikosi kazi maalum kitakachoshirikiana na wenzake wa UDA katika kutekeleza ajenda kumi za makubaliano. Kikosi hicho kitahakikisha utekelezaji kamili wa mapendekezo ya NADCO, kushughulikia masuala ya vijana, haki ya maandamano ya amani, utawala wa sheria, na vita dhidi ya ufisadi.
"Tumeamua kuunda timu hiyo ili kuwezesha utekelezaji wa ajenda ya pamoja kama ilivyopendekezwa katika MOU baina ya ODM na UDA," Kamati ilisema.
Kuhusu ugatuzi, ODM ilitambua kuwa ongezeko la mgao kwa kaunti hadi Ksh bilioni 415 ni hatua nzuri lakini haitoshi. Chama hicho kitaendelea kushinikiza kuongezwa kwa mgao huo hadi angalau Ksh bilioni 450 kama alivyopendekeza Raila Odinga.
"Mgao huo unapaswa kuongezwa hadi angalau Shilingi bilioni 450 au zaidi," ODM ilisema katika tamko lake.
Chama pia kilitoa wito wa kuitishwa kwa kongamano la kitaifa la vizazi mbalimbali litakalolenga kuunda dira mpya ya taifa, hususan kwa vijana.
"Tunaiunga mkono dhati miito ya kuitishwa kwa kongamano la kizazi kwa kizazi, litakalotoa dira mpya kwa taifa letu," Raila alisema.
Pia, ODM ilitangaza kuendeleza uchaguzi wa mashinani na maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa chama hicho, kama njia ya kujenga upya miundo yake ya ndani.
"Tutatumia maadhimisho ya miaka 20 siyo tu kusherehekea mafanikio yetu, bali pia kujipanga kwa siku zijazo katika kuwa chama cha mageuzi," ilisema Kamati.
Licha ya tofauti za maoni zilizokuwepo mwanzoni mwa kikao, ODM ilisema kuwa wajumbe walitoka wakiwa na msimamo mmoja, mshikamano mpya na ari ya kuwatumikia wananchi.
"Tumefikia makubaliano ya pamoja kwa kauli moja—kuendeleza mshikamano, kuimarisha ODM na kusimamia ajenda ya mabadiliko ya taifa letu," ilisistiza Kamati.