
NAIROBI, KENYA, Julai 29, 2025 — Kwa mara ya kwanza kwa muda mrefu, chama cha ODM kinajikuta kwenye mgawanyiko wa wazi, huku sauti za upinzani zikizidi kuibuka kutoka ndani. Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, amezua mjadala mkubwa baada ya kutangaza kuwa chama hicho kiko kwenye hali ya kufa kisiasa, akikitaja kama “Disco Matanga”.
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimeingia kwenye kipindi kigumu zaidi katika historia yake ya miaka 22, huku migawanyiko ya ndani ikiibuka na kuashiria hali ya hatari kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, amesema kuwa chama hicho kimekufa kiutendaji, na hali inayoshuhudiwa sasa ni ya kusubiri mazishi rasmi.
“Kwa sasa tunaishi ndani ya ‘Disco Matanga’ katika ODM. Kimsingi, chama kimekufa, na tunacheza tu tukisubiri siku ya mazishi. Hali ni mbaya, hatua lazima zichukuliwe mara moja,” alisema Amisi.
Ameongeza kuwa pamoja na tofauti za kisiasa zilizopo kati yake na Raila Odinga, bado anamuheshimu kwa nafasi yake katika historia ya taifa, akiwataka vijana wasitumie mitandao ya kijamii kumdhalilisha kiongozi huyo mkongwe.
“Baadhi yetu tunamheshimu Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, japo hatukubaliani naye. Hutaweza kunisikia nikimtusi, kwa sababu anashikilia nafasi ya kihistoria. Lakini vijana wa sasa hawalielewi hilo, wanaishia kumkashifu kwenye mitandao,” alisema Amisi.
Matamshi haya yanajiri wakati makundi mawili yanayoegemea Magharibi mwa Kenya na Nyanza yakionyesha tofauti kali kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa chama hicho.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, hivi karibuni alitangaza kuwa chama hicho hakitamuunga mkono Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027, hatua iliyozua sintofahamu kwani inakinzana na ishara za Raila za kuonyesha uwezekano wa kushirikiana tena na Ruto.
Kauli ya Sifuna imezua mgawanyiko mkubwa, hasa baada ya wabunge wanaomuunga mkono kuandaa mkutano mjini Kakamega, na kutoa wito kwa chama kuunga mkono msimamo wake.
Wakati huo huo, kundi lingine lililojumuisha viongozi kutoka Nyanza, likiongozwa na Mwenyekiti wa ODM kitaifa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, lilifanya mkutano katika eneo la Muhoroni ambapo walimshambulia Sifuna kwa matamshi yake.
“Raila Odinga hajatuagiza tuache mkataba huu. Ukiupinga, husemi kwa niaba ya ODM,” alisema Gavana Wanga kwa msisitizo.
Huku vita hivi vya maneno vikichacha, dalili za kuvunjika kwa chama hicho zinazidi kuongezeka, kwani kwa mara ya kwanza, misimamo ya wazi ya makundi imekuwa ya kugonganisha viongozi wakuu wa chama.
Kwa kutambua hatari inayokikumba chama, Raila Odinga ameanzisha juhudi za kuleta maridhiano kwa kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Usimamizi wa Chama (CMC) ili kujadili mgogoro unaoendelea na kuweka msimamo wa pamoja.
Wachambuzi wa siasa wanaona hali hii kama kipimo kikubwa kwa ODM kuelekea 2027, hasa ikizingatiwa kuwa chama hicho kimekuwa kinahesabiwa miongoni mwa vyama vya kisiasa vyenye misingi thabiti ya kitaasisi na ufuasi mkubwa.