
MWANAMUME mwenye umri wa makamo ambaye mwezi jana alizuiliwa na walinzi wa rais Yoweri Museveni wa Uganda akijaribu kumkimbilia rais huyo amekiri makosa yake.
Kijana huyo alionekana kuwa na nia ya kumfikia rais Museveni
wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Kawempe Kaskazini lakini kwa
bahati nzuri akazuiliwa na walinda usalama wa rais.
Kulingana na jarida la Daily Monitor, Yoram Baguma, 28, sasa
amekiri mashtaka yake ya kutaka kumshambulia na kumdhuru rais na kuomba
msamaha.
‘Ningependa kuomba radhi
kwa shtaka la kujaribu kumshambulia rais,” Baguma ambaye alikuwa
anazungumza kwa lugha ya Runyankore alisema kupitia kwa mtafsiri wa mahakama.
Jamaa huyo alisomewa mashtaka kwamba mnamo Machi 11 wakati wa
siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo wa Eneobunge la Kawempe North
katika uwanja wa Mbogo, alikiuka maagizo ya kiusalama na kuonyesha nia ya
kumdhuru, kumshambulia na kumkera rais.
Katika video ambayo ilisambazwa mitandaoni, Baguma alionekana
kwenye kasi ya ajabu kuelekea kwa rais Museveni lakini kabla ya kumfikia,
aliweza kuzuiliwa na walinda usalama.
Museveni alikuwa anafanya kampeni kwa mgombea wa chama tawala
cha NRM, Faridah Nambi ambaye hata hivyo aliibuka wa pili baada ya kushindwa na
mgombea wa chama cha upinzani cha NUP, Elias Nalukoola.
Baada ya kukiri mashtaka yake, Baguma alirudishwa rumande
baada ya hakimu kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 30, wakati ambapo Baguma atakuwa
amepata wakili kwani kesi inayomkabili inavutia hukumu ya pili kwa ukubwa
nchini Uganda.