
Kwenye eneo la ujenzi
wa Mradi wa Maji wa Quilonga unaotekelezwa na Shirika la Ujenzi wa Umeme la
China (PowerChina) mashariki mwa Luanda, mji mkuu wa Angola, wafanyakazi
wanaendelea na majukumu yao kwa mpangilio mzuri.
Figueira Kalunga, fundi anayesimamia usalama, huzunguka eneo
la ujenzi akikagua kwa makini kofia, mikanda ya usalama na vifaa vingine vya
kujikinga vinavyotumiwa na wafanyakazi.
Kalunga amehusika katika miradi kadhaa ya PowerChina tangu
mwaka 2017, akiianza kazi yake kama fundi chuma.
“Ninajivunia kuwa sehemu ya mradi huu unaoboresha maisha ya
watu. Hauleti tu ajira kwa Wamangola wengi, bali pia utanufaisha idadi kubwa ya
wakazi mara utakapo kamilika,” alisema.
Kwa muda mrefu, Luanda imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa
wa maji kutokana na ukame, miundombinu ya zamani na uwezo mdogo wa kusafisha na
kusambaza maji.
Antonio Fernandes Rodrigues Belsa da Costa, katibu wa
serikali anayehusika na maji katika Wizara ya Nishati na Maji ya Angola,
alisema katika eneo la mradi kwamba mji mkuu bado una upungufu wa maji wa hadi
asilimia 50, huku baadhi ya maeneo yakipata maji mara moja tu kila baada ya
siku mbili au tatu.
Kwa mujibu wa meneja wa mradi Zhang Qiang, Mradi wa Maji wa
Quilonga unahusisha kituo cha kusukuma maji ghafi chenye uwezo wa lita 570,000
za ujazo kwa siku, bomba la kusafirisha maji ghafi lenye urefu wa kilomita
12.5, kiwanda cha kusafisha maji chenye uwezo wa lita 500,000 za ujazo kwa
siku, pamoja na vituo vitano vya usambazaji.
Ujenzi unaendelea kulingana na ratiba, na mara utakapo kamilika, mradi huu utapunguza kwa kiwango kikubwa uhaba sugu wa maji mashariki mwa Luanda, alisema Zhang.
Zhang Peng, mhandisi mkuu, alisema kituo cha kusukuma maji
kilichoko kwenye kingo za Mto Kwanza kilikumbana na changamoto nyingi za ujenzi
kutokana na ardhi yenye unyevunyevu na msingi unaohitaji kuchimbwa kwa kina.
“Kwa kutumia mbinu bunifu za uhandisi, tumeweza kuweka
msingi imara kwa ajili ya muundo mkuu,” alisema.
Zaidi ya ujenzi, timu ya mradi imejitahidi kupunguza tofauti
za kanuni na viwango vya kiufundi kati ya China na Angola.
Pia wamesaidia kukuza maelewano ya kitamaduni kwa kuandaa
shughuli mbalimbali, kutoa mafunzo ya lugha, na kuajiri wahandisi wa kienyeji
waliopata masomo nchini China, hatua ambayo inasaidia kuongeza ushirikiano na
uelewa kati ya wafanyakazi.
Helmano Adriano, msimamizi wa manispaa ya Bom Jesus ambako
mradi huu unatekelezwa, alisifu kujitolea kwa PowerChina kusaidia jamii kupitia
miradi ya kijamii kama vile ujenzi wa mifumo ya maji ya kunywa, usakinishaji wa
mtandao wa umeme, na kusaidia mipango ya kijamii ambayo inanufaisha moja kwa
moja maelfu ya wakazi.
“Mradi wa Maji wa Quilonga utaimarisha kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa maji jijini na kimsingi kufunga pengo lililopo. Tunaamini kwamba ifikapo mwaka 2026, mara utakapokamilika, utapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upungufu wa maji Luanda,” alisema Belsa da Costa.