Mbunge wa Kikuyu ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah amefichua kwamba mwaka wa 2018 wakati kuliibuka tofauti za kisiasa katika chama cha Jubilee, rais mstaafu Uhuru Kenyatta aliwahi mpigia simu na kumgombanisha kwa Zaidi ya saa moja na dakika 30.
Akizungumza katika mahojiano na blogu ya Kenyan Historian kwenye YouTube, Ichung’wah alisema kwamba mwanzoni mwa mwaka 2018 baada ya Handshake ya Kenyatta na Odinga, mgawanyiko ulishuhudiwa katika chama tawala kipindi hicho na kusababisha baadhi ya wanachama kuegemea upande wa rais na wengine upande wa naibu rais William Ruto kipindi hicho.
Kwa wakati mmoja, Ichung’wah alihadithia kwamba Kenyatta aliwahi mpigia simu Jumapili moja adhuhuri na kumgombansha kwa muda mrefu kisa kuandika mitandaoni kwamba kakake rais alihusika kwenye sakata la sukari yenye sumu lakini pia kuonekana kusimama tisti na William Ruto.
“… Nilitoka kanisani nikapata alinipiga, nikampigia na alipokea simu akaanza na maneno matatu ‘Ichung’wah, uliamua kupigana na mimi?’ kwa Kikuyu…. Na naweza sema tulikuwa na mazungumzo kwa saa moja na nusu kwa simu,” Ichung’wah alikumbuka.
Ichung’wah alisema kwamba tatizo lake na Kenyatta lilikuwa kwamba ameungana na Ruto kufanya siasa badala ya kufanya kazi naye ili kuilinda manifesto yake.
Hata hivyo, Ichung’wah alisema kwamba katika mazungumzo hayo alimuambia Kenyatta moja kwa moja kwamba hata kama angemtaka kukoma kumuunga Ruto mkono haingewezekana.
“Nilimwambia kwamba niko tayari kukusikiliza lakini ni lazima nikuambie kwamba mimi ni mtu mkweli, kuna vitu vingi nimesema nchini kote tukiwa na Ruto na siwezi vikanusha. Pengine ukinipa sababu nzuri kwa nini nisifanye kazi na Ruto,” alisema.
Kutoka hapo, Ichungw’ah alisema kwamba hakuweza kuzungumza na Uhuru tena hadi mwaka 2019.
Mbunge huyo mtetesi mkali wa sera za Ruto alisema kwamba wakati mmoja Uhuru alikuja tena kumpigia simu usiku mkuu akimfokea kwamba anavuruga serikali yake.
“Na huo ndio usiku Uhuru Kenyatta aliniambia atanivunja, atanimaliza. Na katika ujinga wangu nilimwambia kwamba rais tafadhali usinitishe. Nilisikia akigonga meza akisema kwamba sijakutishia ila nakwambia… Wakati vitisho vilizidi nilikata simu na nikamblock na hiyo ndio ilikuwa mara ya mwisho kuongea na Uhuru Kenyatta,” Ichung’wah alisema.