
Rais wa Kenya william Ruto sasa anasema kwamba hana wasi wasi na wapinzani wanaojaribu kuwagawanya wakenya.
Akizungumza katika ziara ya siku tatu ilioanza leo Jumanne kasikazini mwa Kenya amesema kwamba wapinzani wanaojaribu kuwagawanya wakenya kwa misingi ya kikabila, Dini, Maeneo au hata masikini na matajiri watafeli na hawataamini.
"Wale wanajaribu kutugawanya wataanguka na wataanguka kabisa. Mara wanataka kutugawanya kwa misingi ya kikabila, mara wagawanye watu wa Bara na watu wa Pwani, wanagawanya watu wa mlima na wa bonde, mara watu wale wako na mshahara na wale hawana. Hawa watu mimi nawaambia hawana mipango au maono yoyote katika Taifa la kenya. Na nataka kuwahakikishia kwamba hawatafaulu kugawanisha taifa letu. Hawana kazi ingine ya kufanya wanataka kututenganisha," alisema Rais William Ruto.
Akizungumza amewahakikishia wenyeji wa kasikazini mwa Kenya kwamba mkoa huo hautatengwa chini ya uwongozi wake bali watakua kama wakenya wengine.
Rais ameahidi kutatua swala ambalo limekuwepo la ugumu wa kupata vitambulisho katika eneo hilo, Rais ameahidi kuondo utafiti na uchunguzi ambao hufanywa kabla mtu kupata kitambulisho cha Taifa katika eneo hilo ili kuwarahisishia shughuli wenyeji.
" Enzi za watu wa kasikazini mwa Kenya kuishi kama watu ambao si wakenya zimeisha. watu wa mkoa huu pia ni watu kama wale walioko katika sehemu yoyote ya Kenya, ndio maana lazima tuweke stima, maji, barabara na watoto wa eneo hili wanufaike kama watoto wengine wanaotoka sehemu zingine za taifa la Kenya.
"Kesho nitakuwa na sherehe kubwa ya kuondoa maneno ya kupigwa msasa kwa wale watu ambao wanataka kupata kitambulisho cha Kenya. Hilo ni jambo la kufanya mara moja na tunakamilisha," Rais Ruto aliwaelezea wenyeji.
Rais amewahakikishia wenyeji kwamba hilo ni Jukumu lake na atatimiza hiyo ahadi ili kuhakisha Kenya imeungana na ni moja.