logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Msiba Maradufu: Mbunge Malulu Injendi Alimpoteza Kakake Saa Chache Kabla Ya Kufariki

Familia ya marehemu Malulu Injendi inakabiliwa na msiba mzito baada ya kifo cha mbunge huyo na kaka yake mkubwa.

image
na Samuel Maina

Yanayojiri18 February 2025 - 08:03

Muhtasari


  • Kifo cha Malulu kilitokea saa chache tu baada ya kaka yake, Samuel Injendi, kufariki Jumapili, Februari 16, 2025, katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega.
  • Familia ilikuwa imepanga harambee  Februari 19, ili kuchangisha fedha za kugharamia bili za hospitali na maandalizi ya mazishi ya Samuel.

Mbunge wa Malava Malulu Injendi

Familia ya marehemu Moses Malulu Injendi, inakabiliwa na msiba mzito baada ya kifo cha ghafla cha mbunge huyo wa Malava na kaka yake mkubwa, Samuel Injendi, ndani ya kipindi kifupi cha saa kadhaa.

Mheshimiwa Malulu Injendi alifariki dunia Jumatatu, Februari 17, 2025, akiwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, ambako alikuwa akipokea matibabu.

Kifo chake kilitokea saa chache tu baada ya kaka yake, Samuel Injendi, kufariki Jumapili, Februari 16, 2025, katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega.

Samuel, ambaye aliaga na umri wa miaka 80 alikuwa afisa mstaafu wa magereza, na alikuwa akiugua kwa muda kabla ya kifo chake.

Familia ilikuwa imepanga kufanya harambee Jumatano, Februari 19, ili kuchangisha fedha za kugharamia bili za hospitali na maandalizi ya mazishi ya Samuel, yaliyopangwa kufanyika Jumamosi, Februari 22.

Hata hivyo, mipango hiyo sasa inahitaji kurekebishwa ili kushughulikia vifo vya ndugu hao wawili.

Malulu Injendi amehudumu kama Mbunge wa Malava kwa muhula wake wa tatu mfululizo tangu 2013. Aidha, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu na Utafiti, ambapo alijitahidi kuboresha sekta ya elimu nchini.

Kufuatia kifo chake, viongozi wa ngazi za juu nchini wakiongozwa na Rais William Ruto, Naibu Rais Kithure Kindiki, na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wameeleza huzuni yao kwa kumpoteza kiongozi shupavu na mwakilishi wa wananchi aliyejitolea kwa dhati.

Rais Ruto, katika rambirambi zake, alimtaja Malulu Injendi kama kiongozi mwenye dira aliyewahudumia wananchi wa Malava kwa kujitolea.

"Nimehuzunishwa sana na kifo cha rafiki na mwenzangu, Mheshimiwa Malulu Injendi. Alikuwa kiongozi mwenye msimamo thabiti aliyewatumikia wananchi wake kwa uaminifu na uadilifu. Alijitahidi kuhakikisha kuwa fursa za elimu zinapatikana kwa wote. Tunawaombea faraja familia yake, marafiki na watu wa Malava katika kipindi hiki kigumu. Pumzika kwa amani, rafiki yangu," alisema Rais Ruto.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, alieleza masikitiko yake kwa kumpoteza kiongozi aliyekuwa rafiki wa wengi na mzalendo wa kweli.

"Kifo kimetunyang’anya kiongozi mahiri na rafiki wa wengi. Tunawaombea neema na amani familia yake pamoja na wananchi wa Malava katika kipindi hiki cha majonzi," alisema Kindiki.

Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alimtaja Injendi kama mtu mtulivu na mwenye kujali maslahi ya jamii yake.

"Mheshimiwa Malulu Injendi alikuwa kiongozi makini na mcha Mungu. Alikuwa rafiki yangu wa karibu wakati tulipohudumu pamoja katika Bunge la 12. Kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia yake, watu wa Malava, na jamii ya eneo la Magharibi mwa Kenya. Nawapa pole za dhati familia yake na watu wa Malava. Mungu ampumzishe kwa amani," alisema Gachagua.

Kwa sasa, familia ya Injendi inakabiliwa na changamoto ya kupanga mazishi ya ndugu hao wawili kwa wakati mmoja, huku jamii ya Malava ikiomboleza na kutoa pole kwa familia katika kipindi hiki cha majonzi.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved