
Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii, Dkt. Alfred Mutua, ameweka wazi jinsi mchakato wa uajiri wa kazi za nje ya nchi unavyofanywa chini ya mpango wa Kazi Majuu, akisisitiza kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha uwazi na ufanisi katika zoezi hilo.
Akizungumza Jumatano baada ya kuzindua zoezi la kuwasajili wanaotafuta ajira katika kanisa la Jesus Winner Ministry, Roysambu, Mutua alisema kuwa wizara yake inashirikiana na mashirika ya uajiri yaliyoidhinishwa pamoja na waajiri wa kigeni kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata kazi zenye hadhi katika sekta mbalimbali.
"Ajira tunazotoa zinahusisha sekta muhimu kama afya, hoteli, ujenzi, uchukuzi, na huduma za baharini. Tuna hakika kuwa kwa kushirikiana na waajiri wa kigeni, tutatoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana wa Kenya," alisema Mutua.
Waziri huyo alieleza kuwa serikali imeweka mfumo wa uwazi wa kuajiri watu, ambapo waombaji wa kazi lazima wapitie mashirika rasmi ya uajiri yaliyoidhinishwa na serikali.
"Hatufanyi mambo kiholela. Tumehakikisha kuwa kuna mfumo rasmi wa uajiri, na waombaji watachujwa ipasavyo ili kupata wale walio na vigezo vinavyohitajika kwa kazi wanazoomba," alieleza.
Kwa mujibu wa Mutua, serikali pia itaharakisha upatikanaji wa hati muhimu kama pasipoti kwa wale watakaofaulu katika mchujo huo.
Mbali na kupata nafasi za ajira, wale watakaofaulu katika mchakato wa uajiri watapokea msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ili kurahisisha mpito wao kwenda kufanya kazi nje ya nchi.
"Tunataka kuhakikisha kuwa Wakenya wanaokwenda kufanya kazi nje hawakumbwi na changamoto zisizo za lazima. Serikali itawasaidia kupata pasipoti haraka na pia msaada wa kifedha ili waweze kuanza maisha yao mapya kwa urahisi," alisema Waziri Mutua.
Aliongeza kuwa ajira hizi zitawapa Wakenya fursa ya kuboresha maisha yao na pia kuinua uchumi wa nchi kupitia fedha watakazotuma nyumbani kama remittance.
Mutua aliwasihi Wakenya kuchangamkia fursa hii na kufika kwenye kituo cha uandikishaji ili kujisajili kwa nafasi hizo. Alisema kuwa zoezi hilo litaendelea kesho katika ukumbi huo huo wa Jesus Winner Ministry, Roysambu.
"Ninawahimiza vijana wenye vigezo wajitokeze kwa wingi. Hii ni fursa ya kubadilisha maisha yenu. Vilevile, naomba vyombo vya habari viendelee kueneza habari hizi ili Wakenya wengi zaidi wanufaike," alihitimisha.
Ingawa mpango huu umewapa matumaini maelfu ya Wakenya wanaotafuta kazi, umepokelewa kwa hisia mseto. Wakati baadhi ya wananchi wanausifu kwa kupunguza ukosefu wa ajira, wengine wameeleza wasiwasi wao kuhusu mazingira ya kazi na usalama wa Wakenya wanaopelekwa nje ya nchi.
Baadhi ya wakosoaji wanasema kuwa serikali inapaswa kuimarisha uchumi wa ndani ili kutoa ajira za kutosha badala ya kutegemea nafasi za kazi za ng’ambo. Aidha, kumekuwa na malalamiko kuhusu visa vya unyanyasaji kwa Wakenya wanaofanya kazi nje, hasa katika mataifa ya Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, Mutua alisisitiza kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti ya kulinda haki za wafanyakazi wote wanaoajiriwa kupitia mpango wa Kazi Majuu, akiahidi kwamba serikali itaendelea kufuatilia ustawi wao hata baada ya kuondoka nchini.
Mpango wa Kazi Majuu ni mojawapo ya juhudi za serikali za Rais William Ruto kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata nafasi nyingi za ajira, si ndani ya nchi pekee bali pia katika soko la kimataifa.