logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Utuletee chapati 3 kila mtu, soda nitasimamia! - 'Kibaki' wa Kiambu amwagiza rais Ruto kabla ya ziara ya Mt Kenya

Njau alimwomba Ruto kuwaletea chapati wakati wa ziara yake, akiahidi yeye binafsi atagharamia soda kwa wenyeji.

image
na Samuel Maina

Yanayojiri29 March 2025 - 11:12

Muhtasari


  • Mbali na kumkaribisha, Njau alitumia fursa hiyo kumwomba Ruto kujenga choo cha umma katika eneo la Kirigiti ili kusaidia wafanyabiashara wa soko.
  • Aidha, alimuomba Rais aambatane na Naibu Rais Kithure Kindiki wakati wa ziara hiyo, akisema wakazi hawajamuona kwa muda mrefu.

Bw Samuel Njau amemkaribisha rais William Ruto katika eneo la Mt Kenya

Bw. Samuel Njau Gicheru, mkazi wa Kirigiti katika Kaunti ya Kiambu, amemkaribisha Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya kabla ya ziara yake iliyopangwa wiki ijayo.

Njau, ambaye anafanana sana na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, alitoa ujumbe wake kwenye video huku akimwiga Kibaki kwa sauti na mtindo wake, akieleza furaha ya wenyeji kuhusu ujio wa Rais.

Akizungumza kwenye video hiyo iliyosambazwa mtandaoni, Njau alisema wakazi wa Kirigiti wanamsubiri kwa hamu Rais Ruto, akimkumbusha kuwa eneo hilo ndilo lililoshuhudia mkutano wake wa mwisho wa kampeni kabla ya uchaguzi wa 2022.

Mbali na kumkaribisha Rais, Njau alitumia fursa hiyo kumwomba Ruto kujenga choo cha umma katika eneo la Kirigiti ili kusaidia wafanyabiashara wa soko.

"Habari, Rais Ruto. Habari yako? Tunaskia unakuja Mlima Kenya, na sote tuko na furaha na tunakusubiri kwa hamu. Niko hapa Kirigiti, mahali ulifanya kampeni yako ya mwisho, na tunakungoja kwa hamu," alisema Njau.

Aidha, alimuomba Rais aambatane na Naibu Rais Kithure Kindiki wakati wa ziara hiyo, akisema wakazi hawajamuona kwa muda mrefu. 

"Hapa Kirigiti, hatuna mambo mengi. Sisi ile kitu tunataka ni choo cha umma, maana huwa tunaenda huko nyuma ya maduka na soko, na kuna kina mama. Hiyo inatosha," alisema.

 Katika hali ya utani, Njau alimwomba Ruto kuwaletea chapati wakati wa ziara yake, akiahidi yeye binafsi atagharamia soda kwa wenyeji. 

"Lakini pia ni muhimu, wakati ule unakuja, utuletee Kindiki tumsalimie, maana hatujamuona. Na hiyo kitu ingine, ni lazima utuletee chapati, kila mtu tatu. Mambo ya soda mimi nitasimamia. Si namna hiyo?" aliongeza. 

Ujumbe wa Njau unakuja wakati ambapo Rais William Ruto anapanga ziara yake katika maeneo mbalimbali ya Mlima Kenya kuanzia Aprili 1.

Rais Ruto anatarajiwa kuanza ziara yake ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya, ikiwa ni mara yake ya kwanza kurejea katika eneo hilo baada ya miezi sita. Ziara yake inajiri wakati wa msisimko wa kisiasa, kufuatia kung’olewa kwa aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua.

Ratiba yake inajumuisha ziara katika kaunti saba, ambapo atakutana na wakazi, kukagua miradi ya maendeleo, na kushughulikia masuala muhimu ya eneo hilo.

Ratiba ya Ziara:

Jumanne, Aprili 1: Kaunti za Laikipia na Nyeri 

Jumatano, Aprili 2: Kaunti za Meru na Kirinyaga

Alhamisi, Aprili 3: Kaunti za Nyandarua na Murang’a

 Ijumaa, Aprili 4: Kaunti ya Tharaka Nithi

 Mlima Kenya limekuwa ngome muhimu ya kisiasa, na ziara ya Ruto inaonekana kama juhudi za kudumisha uungwaji mkono wake wakati hali ya kisiasa inabadilika. Masuala makuu yanayotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na changamoto za kiuchumi, kilimo, na mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea.

 Ziara hiyo inafuatiliwa kwa karibu, huku wachambuzi wakitabiri jinsi itakavyobadili mwelekeo wa siasa za eneo hilo kufuatia kung’olewa kwa Gachagua.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved