logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kizaazaa huku wabunge wawili wanawake wakipimana nguvu nje ya bunge, fahamu kilichotokea

Wawili hao walinaswa wakibishana vikali kabla ya kugeuza majibizano kuwa fujo.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri09 April 2025 - 11:55

Muhtasari


  • Juhudi za baadhi ya wabunge wa kike kuwatuliza hazikufua dafu, huku mzozo ukizidi kuongezeka.
  • Baada ya tukio hilo, Umulkheir alitoa taarifa rasmi akieleza masikitiko yake juu ya yaliyotokea.

Wabunge wawili wa kike wakipigana nje ya bunge

Vurugu zilitokea katika majengo ya Bunge Jumanne baada ya wabunge wawili wa kike kushiriki katika ugomvi wa wazi ulionaswa na kamera, tukio lililozua taharuki ndani na nje ya Bunge.

Wabunge walioshiriki katika mzozo huo ni Mwakilishi Wamawake aliyechaguliwa na chama cha ODM, Umulkheir Harun, na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Falhada Iman.

Katika video iliyotazamwa na Radio Jambo, wawili hao walinaswa wakibishana vikali kabla ya kugeuza majibizano kuwa fujo.

Juhudi za baadhi ya wabunge wa kike kuwatuliza hazikufua dafu, huku mzozo ukizidi kuongezeka.

Mbunge mmoja alisikika akiomba usaidizi kutoka kwa wenzake waliokuwa wakiangalia kutoka mbali, huku mwingine akiwasihi waache kurekodi tukio hilo.

Afisa wa Usalama wa Bunge aliingilia kati na kufanikisha kuwatenganisha. Hata hivyo, hata baada ya kutulizwa, wawili hao waliendelea kurushiana maneno ya matusi.

Baada ya tukio hilo, Umulkheir alitoa taarifa rasmi akieleza masikitiko yake juu ya yaliyotokea.

"Leo, tukio la kusikitisha limetokea katika viwanja vya Bunge—hali ambayo naijutia kwa dhati kama Mbunge na pia kama mama," alisema.

Alithibitisha kuwa tayari amepeleka malalamiko rasmi kwa mamlaka husika.

"Nimewasilisha malalamiko ya kushambuliwa kwa taasisi husika," aliongeza.

Umulkheir alilaani tukio hilo na akasisitiza kuwa hapaswi wala haungi mkono mienendo isiyo ya heshima.

"Ninajutia sana tukio hili na nataka kusisitiza kwamba siungi mkono wala kuruhusu aina yoyote ya tabia isiyo ya nidhamu," alisema. "Ingawa sitatoa maoni zaidi kwa sasa, ninasalia kuwa na dhamira ya dhati ya kuzingatia viwango vya heshima na hadhi vinavyotegemewa kutoka kwangu na taasisi yetu, hasa kama mwanamke Mwislamu."

Alihitimisha kwa kutoa wito wa maadili na heshima katika ulingo wa siasa.

"Ulingo wa kisiasa una changamoto nyingi, lakini hakuna sababu ya kuhalalisha tabia zinazopunguza hadhi ya kazi yetu," alisisitiza. "Natumai kwamba kwa pamoja tutaweza kuendeleza mazingira yenye heshima na mazungumzo ya kujenga katika siku zijazo."

Chanzo cha ugomvi huo bado hakijabainika, na haijulikani kama hatua za kinidhamu zitachukuliwa.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved