
Aliyekuwa Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala, ameachiliwa kutoka rumande katika Kituo cha Polisi cha Eldama Ravine baada ya kushikiliwa tangu Jumatano. Hakushtakiwa kwa kosa lolote.
Malala alikamatwa katika Shule ya Kirobon, Nakuru, alipokuwa ameandamana na kikundi cha maigizo cha Shule ya Upili ya Butere kwa mazoezi ya tamthilia Echoes of War, ambayo yeye ndiye mwelekezi.
Kulingana na Malala, aliwasili shuleni hapo majira ya saa kumi na moja na nusu jioni kwa ajili ya mazoezi, lakini alikuta maafisa wa usalama wakiwa langoni wakizuia gari lake kuingia.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuachiliwa, Malala aliwasifu wanafunzi wa Butere Girls kwa kuamua kususia onyesho hilo baada ya kunyimwa mwelekezi wao.
“Ninasema kuwa wasichana hao ni mashujaa wa taifa hili. Wanastahili kuenziwa na majina yao yaandikwe katika historia ya nchi hii,” alisema.
Akiwa bado korokoroni, Malala alihojiwa kwa simu na redio moja na kuwalaumu maafisa wa tamasha la drama kwa kuwakosesha wanafunzi fursa ya kuonyesha kazi yao.
“Ilikuwa hatua ya kishujaa kwa wasichana hao kwa sababu wasingeweza kutumbuiza bila hadhira, mapambo, mavazi ya jukwaani na waelekezi wao. Hii si haki, na naamini wale waliohusika lazima wawajibishwe kwa kuwakosesha wanafunzi haki yao ya kushiriki shughuli ya kisanii,” alisema.
Ripoti zinaeleza kuwa wanafunzi hao waliingia jukwaani, wakaimba wimbo wa taifa kisha wakaondoka kwa maandamano wakitaka mwelekezi wao awepo.
Inadaiwa pia kuwa walinyimwa vifaa vya msingi kama maikrofoni, mapambo na vifaa vingine vya jukwaani tofauti na shule nyingine, hali iliyowalazimu kususia kabisa.
Licha ya changamoto hiyo, Malala aliwahimiza wanafunzi waendelee kuwa na matumaini na ujasiri katika safari yao ya kisanaa.
Tamthilia ya Echoes of War
inazungumzia masuala ya kisasa kama teknolojia, utawala na haki za kijamii,
hasa kwa kizazi cha Gen Z. Inasimulia taifa linalojijenga upya baada ya vita
kwa uongozi wa vijana, na inakosoa nafasi ya mitandao ya kijamii katika uundaji
wa sera na maisha ya kiraia.