logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Tamthilia ya 'Echoes of War' kuigizwa na watu wazima - Cleophas Malala

Malala ametangaza kuwa tamthilia yake tata Echoes of War sasa itaigizwa na watu wazima.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri17 April 2025 - 10:56

Muhtasari


  • Malala alisema kwamba maandishi ya tamthilia hiyo yatachapishwa mtandaoni hivi karibuni ili kuwapa Wakenya wote fursa ya kushiriki.
  • Malala pia aliwatetea wanafunzi wa Butere Girls kufuatia ukosoaji aliopokea kwa kuwashirikisha katika tamthilia hiyo.

Cleophas Malala

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega na Katibu Mkuu wa zamani wa UDA, Cleophas Malala, ametangaza kuwa tamthilia yake tata Echoes of War sasa itaigizwa na watu wazima.

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen TV siku ya Jumatano usiku, Malala alisema kwamba maandishi ya tamthilia hiyo yatachapishwa mtandaoni hivi karibuni ili kuwapa Wakenya wote fursa ya kushiriki.

“Tutaweka maandishi ya tamthilia hiyo kwenye mitandao ya kijamii ili yeyote anayevutiwa aweze kuyapakua, kuiigiza na kuipakia kwenye TikTok,” alisema.

“Kupitia njia hii, tutagundua vipaji kutoka maeneo yote ya nchi—hata yale ya pembezoni. Hii ni tamthilia ya Wakenya na itachezwa na wasanii wa hapa nchini.”

Hata hivyo, licha ya hatua ya kuitoa kwa watu wazima, Malala alisisitiza kuwa wanafunzi wa shule ya wasichana ya Butere waliopaswa kuiigiza tamthilia hiyo kwenye Tamasha la Kitaifa la Drama na Filamu, wanastahili kupewa heshima yao.

“Tutaiendeleza tamthilia hii na waigizaji watu wazima, lakini hatuwezi kuwasahau mabinti wa Butere. Hao ni mashujaa. Sehemu ya mapato ya tamthilia hiyo lazima iwafikie, kwa sababu wataandikwa katika historia,” alisema.

Malala pia aliwatetea wanafunzi hao kufuatia ukosoaji aliopokea kwa kuwashirikisha katika tamthilia hiyo. Alifananisha hatua hiyo na tamthilia ya kihistoria ya Afrika Kusini, Sarafina, akieleza kuwa vijana wamekuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi.

“Hakuna tatizo kwa wanafunzi kushiriki kwenye masuala ya kisiasa au kuunda mustakabali wao kupitia sanaa. Wao ni sehemu ya safari ya mabadiliko,” aliongeza.

Hata hivyo, wanafunzi wa Butere hawakuweza kuonyesha igizo hilo wakati wa tamasha huko Nakuru, baada ya vurugu kuzuka na walinzi kuwazuia waandishi wa habari na umma kuingia katika Shule ya Wasichana ya Kirobon.

Katika mahojiano tofauti na kituo cha habari, Malala alifafanua kuwa wazo la tamthilia hiyo lilichochewa na maandamano ya kizazi cha Gen-Z mnamo Juni 2024.

“Nilianza kulifikiria wazo hili mara tu baada ya maandamano ya Gen-Z. Mimi siandiki tamthilia kwa misingi ya mtazamo wangu binafsi wa maisha. Ninaandika nikichochewa na matukio yanayoendelea katika jamii yetu,” alisema.

“Itakuwa ni kosa mtu kudai kwamba naandika tamthilia kwa ajili ya kulipiza kisasi au kutangaza ajenda ya kisiasa. Sifanyi hivyo kabisa.”


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved