logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Aliyekuwa gavana Meru Kawira Mwangaza aonyesha ujuzi wa kukamua mwezi baada ya kupoteza kiti

“Nilijua kukamua kwa mkono nikiwa darasa la pili. Zamani zile hakukuwa na mashine,” alisema.

image
na Samuel Maina

Yanayojiri20 April 2025 - 11:56

Muhtasari


  • Mwangaza,ameonekana kujielekeza kikamilifu kwenye kazi za nyumbani na mashambani baada ya kuondolewa rasmi afisini mwezi uliopita.
  • Mwangaza alionekana akikamua kwa kutumia mashine na pia kwa mikono, akionyesha ujuzi aliouzoea tangu akiwa mchanga.

Kawira Mwangaza aonyesha ustadi wake katika kukamua maziwa, mwezi mmoja baada ya kutimuliwa

Aliyekuwa Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza, ameonekana kujielekeza kikamilifu kwenye kazi za nyumbani na mashambani baada ya kuondolewa rasmi afisini mwezi uliopita.

Mnamo katikati ya mwezi Machi, Mwangaza alipata pigo kubwa baada ya Mahakama Kuu kuthibitisha uamuzi wa Seneti wa kumuondoa madarakani, ikisema kuwa mchakato huo ulikuwa ndani ya mipaka ya kikatiba.

Siku ya Jumamosi, mwanasiasa huyo alichapisha picha na video kwenye mtandao wa Facebook, zikimuonesha akihusika katika shughuli za kukamua maziwa kwenye banda la ng’ombe.

“Jioni njema. Mama ni mama. Gavana ni mama. #MaziwaPesa,” aliandika chini ya picha hizo.

Katika video ya moja kwa moja, Mwangaza alionekana akikamua kwa kutumia mashine na pia kwa mikono, akionyesha ujuzi aliouzoea tangu akiwa mchanga.

“Nilijua kukamua kwa mkono nikiwa darasa la pili. Zamani zile hakukuwa na mashine,” alisema.

Mwangaza aliongeza kuwa alipokuwa mdogo, alikuwa akikamua ng’ombe wa kienyeji, na alieleza kazi hiyo kuwa ya kuvutia na yenye tija.

“Wakati huo nilikuwa nakamua ng’ombe wa kienyeji. Ni kazi nzuri sana,” alieleza kwa bashasha.

Alipoulizwa kuhusu mipango yake ya kusherehekea Pasaka, Mwangaza alisema kuwa anatarajia kuuza maziwa ili apate pesa za kumfurahisha mumewe Murega Baichu katika msimu huo wa sherehe.

“Nauza maziwa nipate hela za kumfurahisha Murega wakati wa Pasaka,” alisema kwa tabasamu.

Mwezi uliopita, Mahakama Kuu ilisema kuwa Seneti haikuvunja Katiba katika hatua yake ya kumuondoa Mwangaza, na ikatupilia mbali madai kuwa mchakato huo ulikumbwa na dosari.

“Mahakama hii imebaini kuwa ombi lililowasilishwa halina mashiko na linatupiliwa mbali. Tangazo la gazeti la serikali la tarehe 21 Agosti 2024 kuhusu kuondolewa kwake linasalia kuwa halali,” alisema Jaji Bahati Mwamuye.

Mahakama pia iliamuru kuwa masharti yote ya kikatiba kuhusu nafasi hiyo wazi yazingatiwe ndani ya muda uliowekwa.

Kuhusu madai ya Mwangaza kuwa Seneti ilikiuka amri ya mahakama, mahakama ilisema kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa maagizo yoyote halali yaliwasilishwa kwa Seneti.

“Seneti haingeweza kukiuka amri ambazo hazikuwasilishwa ipasavyo mbele yake,” ilisomeka sehemu ya uamuzi huo.

Aidha, mahakama ilibainisha kuwa ingawa ushirikishwaji wa umma ni hitaji la kikatiba, katika mchakato wa kumwondoa gavana madarakani, hatua hiyo hufanyika zaidi katika kiwango cha kaunti kuliko katika Seneti.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved