logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Murkomen Awataka Wakenya Wawe na Nidhamu Wakati wa Mashindano ya CHAN

Murkomen alisisitiza kuwa mashindano hayo yatakuwa jukwaa la kuonesha uwezo wa Kenya.

image
na Tony Mballa

Michezo15 July 2025 - 12:39

Muhtasari


  • Serikali pia imeboresha mifumo yake ya uhamiaji na utoaji wa visa ili kurahisisha ujio wa wageni na ujumbe kutoka mataifa ya nje.
  • Murkomen aliwahimiza Wakenya kuunga mkono mashindano hayo kwa kuhudhuria mechi, kuwaelekeza wageni na kuiwakilisha Kenya kwa njia chanya.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewataka Wakenya waonyeshe heshima na ukarimu wakati taifa linajiandaa kuandaa mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwezi Agosti.

Murkomen alisisitiza kuwa mashindano hayo yatakuwa jukwaa la kuonesha uwezo wa Kenya katika michezo na ukarimu mbele ya hadhira ya kimataifa, huku zaidi ya mataifa 18 ya Afrika yakitarajiwa kushiriki.

“Ninatoa wito kwa kila mmoja kuunga mkono tukio hili muhimu kwa kuhudhuria mechi, kuwaelekeza wageni inapowezekana, na kusaidia kuiwakilisha Kenya kwa sura bora,” alisema Murkomen.

“Kwa zaidi ya mataifa 18 ya Afrika kushiriki, mashindano haya yataonesha umahiri wa Kenya katika michezo na ukarimu mbele ya dunia nzima,” aliongeza.

Wakati wa ukaguzi wa pamoja wa viwanja vya Kasarani na Nyayo akiwa na Waziri wa Michezo Salim Mvurya, Murkomen alisifu Wizara ya Masuala ya Vijana, Uchumi wa Ubunifu na Michezo kwa kukamilisha ukarabati wa viwanja hivyo na maeneo ya mazoezi kwa wakati.

Mawaziri Kipchumba Murkomen na Salim Mvurya

“Jumatatu alasiri, nikiwa na Waziri wa Michezo Salim Mvurya, tulikagua maandalizi ya kiusalama katika viwanja vya Kasarani na Nyayo kwa ajili ya mashindano yajayo ya CHAN 2025,” alisema Murkomen.

“Ninapongeza Wizara ya Vijana, Uchumi wa Ubunifu na Michezo kwa kukamilisha ukarabati wa viwanja na maeneo ya mazoezi kwa wakati.”

Alieleza kuwa Wizara hiyo imeweka mikakati ya kina kuhakikisha usalama wa timu shiriki, maafisa na mashabiki.

“Kama Wizara, tumeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha usalama wa timu shiriki, maafisa na mashabiki. Maandalizi hayo ya kiusalama yanajumuisha usakinishaji wa kamera za CCTV za kisasa viwanjani, maeneo ya kuingia yenye udhibiti, mikakati ya kudhibiti umati, timu za kukabiliana na dharura, na uwepo wa maafisa wa usalama kwa wingi katika maeneo ya mashindano,” alifafanua.

Serikali pia imeboresha mifumo yake ya uhamiaji na utoaji wa visa ili kurahisisha ujio wa wageni na ujumbe kutoka mataifa ya nje.

Murkomen aliwahimiza Wakenya kuunga mkono mashindano hayo kwa kuhudhuria mechi, kuwaelekeza wageni na kuiwakilisha Kenya kwa njia chanya.

“Tuionyeshe dunia uwezo wetu—si tu kwenye michezo, bali pia katika ukarimu na utu,” alisema. Mashindano hayo yakikaribia kuanza, Wakenya wanahimizwa kujitokeza kwa wingi na kufanya tukio hilo kufana.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved