
NAIROBI, KENYA, Jumatano, Julai 24, 2025 — Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka, Harambee Stars, Benni McCarthy, ameonyesha imani kubwa kwa kikosi chake huku maandalizi ya kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024 yakiendelea kwa kasi katika uwanja wa Nyayo.
McCarthy, ambaye ni gwiji wa zamani wa soka kutoka Afrika Kusini, alisema amevutiwa na bidii, maelewano na ari ya wachezaji wake, akisema kuwa kikosi hicho kipo tayari kuwakilisha taifa kwa heshima.
“Nina furaha na kile ninachokiona kambini. Wachezaji wanaonyesha njaa ya mafanikio, maadili ya hali ya juu, na moyo wa kujitolea. CHAN si mashindano rahisi, lakini tuna kikosi chenye uwezo wa kushindana,” alisema McCarthy kwa kujiamini.
Kocha huyo aliongeza kuwa CHAN ni fursa adhimu kwa wachezaji wa ndani kuonyesha uwezo wao na kujitangaza katika medani ya kimataifa.
“Mashindano haya ni kwa wachezaji wetu wa hapa nyumbani. Ni jukwaa la kuonyesha vipaji vyao. Nimefurahishwa na jinsi wanavyopambana kila siku kambini,” aliongeza.
Nahodha wa Harambee Stars Abud Omar (kulia) akabiliana na mshambuliaji wa kikosi hicho cha taifa Ryan Ogam, huku Alphonse Omija akishuhudia/FKF
Hali kambini yautia
Kiungo mahiri wa Gor Mahia, Austin Odhiambo, naye alisisitiza kuwa mazingira kambini ni bora na kila mchezaji anaelewa uzito wa jukumu walilopewa.
“Hali kambini ni nzuri sana. Kila mmoja ana ari na tunajifunza mengi kutoka kwa kocha. Lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vyema na kuonesha kuwa wachezaji wa ligi ya nyumbani wana uwezo mkubwa,” alisema Odhiambo.
Kwa upande wake, beki wa Gor Mahia, Alphonse Omija, alieleza kuwa mazoezi ni makali lakini yenye malengo ya kuandaa kikosi imara na cha ushindani.
“Kocha anatufundisha kwa weledi mkubwa. Kila mchezaji anajituma kwa hali na mali. Tunaamini tunaweza kuleta matokeo mazuri kwa nchi yetu,” alisema Omija.
Harambee Stars inatarajiwa kucheza mechi za majaribio katika wiki zijazo kabla ya kuelekea kwenye fainali za CHAN zitakazoandaliwa mwezi Septemba.
Kenya ipo katika kundi gumu, lakini kwa mtazamo wa sasa, wachezaji na benchi la ufundi wana matumaini makubwa ya kufanya vyema na kuendeleza hadhi ya taifa kwenye soka la Afrika.