
MOMBASA, KENYA, Jumapili, Septemba 28, 2025 — Shabana FC iliendeleza mwanzo wake mzuri wa msimu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bandari katika uwanja wa Mbaraki, goli pekee likifungwa na Brian Michira dakika ya 63.
Shabana FC imeendelea kuonesha uthabiti katika Ligi Kuu ya Kenya baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bandari FC katika Uwanja wa Mbaraki, mjini Mombasa.
Bao la ushindi lilifungwa dakika ya 63 na kiungo Brian Michira, baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Bronson Nsubuga.
Mchuano mkali baina ya mchezaji wa Shabana na wenzake kutoka Bandari/BANDARI
Bandari walijaribu kusawazisha kupitia shambulizi la David Sakwa na shuti kali la Jostine Omwando, lakini kipa wa Shabana, Stephen Otieno, alihakikisha lango lake linabaki salama.
Kocha wa Bandari, Ken Odhiambo, alisema kikosi chake kilikosa kutumia nafasi walizopata. “Katika kandanda, ukikosa nafasi zako, unapata adhabu. Shabana walitumia vizuri nafasi yao moja muhimu,” alisema Odhiambo.
Kwa upande wake, kocha wa Shabana, Peter Okidi, alisifu nidhamu ya wachezaji wake. “Tulijiandaa ipasavyo, tulihitaji alama tatu, na vijana walionyesha kujituma,” alisema Okidi.
Bandari ilimaliza mchezo ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja baada ya William Gitama kuondolewa uwanjani kufuatia majeraha dakika za mwisho.
Kwa ushindi huo, Shabana wamejipatia alama muhimu katika kampeni zao, huku Bandari wakiahidi kurekebisha makosa yao kabla ya mechi dhidi ya Murang’a Seal wiki ijayo. Shabana watakabiliana na Tusker FC katika mchezo wao unaofuata.