
NI mwaka mmoja sasa umepita tangu kifo cha ghafla cha aliyekuwa TikToker mashuhuri humu nchini Brian Chira, shukrani kwa vimbwanga vyake vilivyowakera na kuwapunga wengi kwa viwango sawa.
Baadhi ya waliokuwa marafiki zake wa
karibu wakiongozwa na Obidan Dela waliandaa hafla ndogo ya kumkumbuka Chira
nyumbani kwao.
Dela kupitia ukurasa wake wa TikTok
alichapisha video na picha akijumuika na baadhi ya wanafamilia wa Brian Chira
nyumbani kwao huku wakikariri baadhi ya semi alizopenda kuzitamka mara kwa
mara.
Katika video hiyo, Obidan Dela na Watoto hao
walikuwa wameishikilia picha kubwa ya Brian Chira huku wakikumbuka na kukariri
kauli aliyopenda kuitamka ‘kama wewe si pesa huwezi nipa stress’.
Pia waliimba kwa huzuni wimbo wa Otile
Brown ‘One Call’ ambao ulisheheni sana wakati wa mazishi ya Chira ambapo
ilisemekana ulikuwa moja ya nyimbo alizozipenda pakubwa.
“Yo guys, Obidan Dela hapa, guys, na niko
na Brian Chira na Sophie Njeri Chira Kadogo na wananiambia kama vile Chira
alikuwa anawaambia, ‘Kama wewe si pesa, huwezi ni-stress.’”
Nyota huyo wa zamani wa TikTok alikumbana
na kifo chake baada ya kugongwa na gari usiku wa Machi 16, 2024 wakati wa
msongamano wa barabarani alipokuwa akijaribu kuvuka kuelekea upande mwingine.
Dereva wa gari hilo alikimbia eneo la
tukio, na mwili wake uligunduliwa kando ya barabara mapema asubuhi iliyofuata.
Kufikia wakati anaaga dunia, Chira
alikuwa amekuwa gumzo kwenye programu maarufu ya kushiriki video, akiwa tayari
amevuka idadi ya wafuasi 400,000.