

KATIBU mkuu wa muungano wa wafanyikazi COTU, Francis Atwoli amefichua kwamba likizo ya uzazi kwa wafanyikazi wa kiume humu nchini ni moja ya kazi yake.
Atwoli, kupitia ukurasa wake wa X
alifichua haya alipokuwa akimjibu aliyekuwa gavana wa Makueni profesa Kivutha
Kibwana ambaye alikuwa ametaka COTU kumpa katibu wao likizo ya ubaba.
Kibwana alianza kwa kumhongera Atwoli
kwa kuwa baba mpya mjini, shukrani kwa mkewe Mary Kilobi aliyejifungua mtoto wa
kiume – Atwoli Junior.
“Ninaipongeza kwa moyo wote familia ya
@AtwoliDza kwa ujio mpya katika familia yao. @COTU_K wanapaswa kumpa Katibu
Mkuu wao Likizo ya Ubaba inayostahiki ambapo wanaweza pia kujadili: Je, COTU na
uongozi wa vyama vya wafanyakazi unapaswa kuwa suala la umiliki wa maisha?” Kibwana alihoji.
Akimjibu, Atwoli alianza kwa kufafanua
kwamba amepigania wafanyikazi wa kiume kupata likizo ya ubaba ambayo miaka ya
nyuma haikuwepo.
Atwoli alidokeza kwamba ni kutokana na
juhudi zake ambapo likizo ya ubaba ilisimikwa rasmi kwenye katiba ya Kenya ya
mwaka 2010.
“Kwanza, nimepigania wafanyikazi [wa kiume] wa Kenya kupokea likizo ya uzazi kama sehemu ya kazi yangu kuleta seti tano (5) za sheria za Kazi. Unatambua kwamba sheria hizi na Katiba ya Kenya 2010, kama ilivyo katika Kifungu cha 41, zimempa mfanyakazi Mkenya mamlaka zaidi ya yote katika eneo hili,” alisema.
Kuhusu swali la Kibwana kutaka kujua
kama ukatibu wa COTU ni kazi ya kudumu ya Atwoli, katibu huyo ambaye
ameshikilia uongozi wa COTU kwa takribani miaka 24 alimwambia kwamba hata yeye
amemuona Kibwana akipewa kazi ya kufunza chuo kikuu licha ya kuwa mwanarika
wake na kutaka kujua kama yake pia ni ya kudumu.
“Pili, mimi na wewe ni marafiki wa
umri. Na nilikuona tu ukiteuliwa kuwa profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha
Daystar hapo juzi. Hivi Prof, nieleweshe, taaluma yako inaisha lini? Hivi kweli
profesa anaweza kuacha kusoma, kufundisha na kuandika? Utaacha lini
kushirikisha akili yako?” alimjibu kwa njia ya swali.
Mapema wiki hii, Francis Atwoli,75,
aliripotiwa kukaribisha mtoto na mkewe Mary Kilobi, 40, baada ya kuwa katika
ndoa kwa takribani miaka 7.