
Mtayarishaji wa maudhui maarufu wa Kenya, Azziad Nasenya, amevunja kimya chake kuhusu madai ambayo yamekuwa yakienea mtandaoni yakimhusisha na madeni makubwa ili kufadhili mtindo wake wa maisha.
Akizungumza katika kipinidi cha redio siku ya Jumanne, Azziad alikanusha madai hayo, akiyataja kuwa ni uvumi usio na msingi unaoenezwa mitandaoni.
Alifafanua kuwa haitegemei mikopo ili kufanikisha maisha yake kama mtu mashuhuri, akisisitiza kuwa mafanikio yake ni matokeo ya miaka mingi ya kujituma na kujijenga.
“Hili jambo limekuwa likizungumzwa kwa muda sasa, na ni jambo la kushangaza jinsi mitandao ya kijamii inavyofanya kazi—kama seti kubwa ya filamu ambapo kila mtu anaandika hadithi yake. Hivi majuzi, nimeona simulizi za kuvutia zikienea, na kwa bahati mbaya, mimi ndiye mhusika mkuu wa wakati huu,” alisema Azziad.
Akiweka wazi msimamo wake, alikanusha vikali madai ya kukopa fedha kwa ajili ya maisha yake ya kifahari.
“Sihitaji kufanya hivyo. Watu wanasahau kwamba safari hii haikuanza leo. Nimekuwa nikijiwekeza, nikijituma, na kufanya kazi kwa bidii kwa miaka mingi,” alisema.
Azziad aliongeza kuwa dhana ya kwamba amechukua mikopo ili kufanikisha maisha yake mazuri ni hadithi tu ya mtandaoni ambayo haina mashiko.
“Huu ni uvumi wa muda mfupi, mada inayotrendi tu. Kitu ambacho hakitrendi ni juhudi zangu, uvumilivu wangu, na kazi ngumu niliyoifanya kujenga chapa yangu,” alisisitiza.
Akizungumzia suala la madeni, Azziad alisema anashughulikia masuala yake moja kwa moja na wahusika husika. Alipuuza maneno ya mitandaoni, akisema kuwa uwajibikaji wa kweli hauonyeshwi kwa mijadala ya mtandaoni bali kwa vitendo halisi.
“Mambo yanapohusu fedha, ninaamini katika kuyashughulikia kwa njia sahihi—kupitia vitendo, si kwenye sehemu za maoni. Hicho ndicho ninachofanya,” alisema.
Pia alifafanua kuwa hataruhusu majungu ya mitandao ya kijamii kuathiri maamuzi yake ya kifedha au jinsi anavyoendesha shughuli zake za kibiashara.
“Kama kuna yeyote anayetaka kujua msimamo wangu—ninasimama kwenye ukweli, ukuaji, na vitendo, si kelele zisizo na maana. Mwisho wa siku, cha muhimu ni kushughulikia mambo yako kwa uadilifu na kuruhusu vitendo kuzungumza zaidi ya vichwa vya habari,” alisema kwa msisitizo.
Azziad alihitimisha kwa ujumbe wa kutia moyo kwa vijana wa Kenya, hususan wanawake, akiwahimiza kusimama imara na kutoacha kelele za mitandaoni kuwapotosha.
“Kama umewahi kuhisi kutokueleweka au kazi yako kutiliwa
shaka, kumbuka kwamba ukweli wako hauhitaji mjadala. Acha waseme, acha wabuni
hadithi, lakini mwishowe, kazi yako itaishi zaidi ya maneno ya kupita,”
alisema.