
Mwimbaji maarufu wa Guinea na mshawishi wa mitandao ya kijamii Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P mwishoni mwa juma iliyopita alipiga hatua muhimu kuelekea kufanya mambo iwe rasmi kabisa na mpenzi wake mpya Mariame.
Mwimbaji huyo aliyezingirwa na utata ambaye anajulikana sana kwa maumbile yake ya kipekee, mtindo wake wa kifahari na uhusiano wa zamani na sosholaiti Eudoxie Yao alichukua muda kuwatembelea wakwe zake wapya, ambapo alipokelewa vyema, kabla ya kujitambulisha kwao rasmi.
Katika video na picha zilizosambazwa mtandaoni, Grand P alionekana akitembea kwa fahari na mpenzi wake huku akisindikizwa na kundi kubwa la watu. Pia walionekana wakisimama na kutangamana kwenye mitaa ya mahali inapoaminika kuwa nyumbani kwa Mariame.
"Kutembelea familia yangu nzuri. Asante sana kwa familia yangu ya baadaye kwa ukaribisho,” Grand P aliandika chini ya picha alizochapisha.
Mwimbaji huyo pia alionekana kubeba zawadi kadhaa ili kuwapa wakwe. Zawadi zilijumuisha mafuta ya kupikia, maziwa, kati ya bidhaa zingine za kupikia.
“Mashallah. Mwenyezi Mungu atuangalie,” aliongeza Grand P.
Takriban wiki moja iliyopita, msanii huyo mbilikimo alidokeza nia yake ya kupata mapacha na mpenzi wake mpya Mariame.
Grand P alimtambulisha mpenzi wake mpya, Mariame Kaba, takriban wiki nne zilizopita. Tangu wakati huo, amekuwa akijivunia mahusiano yao na kumtangaza kwa mashabiki wake kwa fahari. Kinachowashangaza wengi kuhusu mpenzi wake mpya ni maumbile yake madogo ya kipekee, ambayo karibu yanafanana na yake.
Katika moja ya machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii, ambapo alikuwa akijigamba kuhusu mpenzi wake, Grand P alishiriki video ya Mariame na kumuita mwanamke mwenye bahati.
Msanii huyo mbilikimo alisema zaidi kuwa Mariame ni mama wa baadaye wa mapacha wake.
"Mwanamke mwenye bahati, mama wa baadaye wa mapacha wa Kaba," aliandika Grand P chini ya video ya Mariame ambayo alichapisha Facebook wiki jana.
Kauli hiyo ilionekana kuashiria matamanio ya mwimbaji huyo ya kupata mapacha na mpenzi wake mpya katika siku za usoni.