
Aliyekuwa Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha, amezungumzia maisha yake baada ya kutimuliwa kwenye baraza la mawaziri na Rais William Ruto mnamo Juni 2024.
Alifichua kuwa hakupata taarifa yoyote ya awali kuhusu kutimuliwa kwake, bali alijifunza habari hizo moja kwa moja kupitia matangazo ya moja kwa moja kwenye televisheni.
"Bishop amehubiri hapa akisema kuwa wakati wa Rais Moi matangazo yalikuwa kwa redio, lakini yetu haikuwa redio, ilikuwa kwa TV. Nilipoangalia, nikasikia baraza la mawaziri lote limefutwa kazi, nikaona watu wamefurahi kila mahali," aliongeza huku akitabasamu.
Nakhumicha, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Afya mnamo 2022, alikuwa mmoja wa maafisa wa serikali waliokumbwa na hasira za umma, huku baadhi ya viongozi wa upinzani na wanaharakati wakimtuhumu kwa kushindwa kusimamia sekta ya afya ipasavyo.
Uamuzi wa Rais Ruto wa kuivunja serikali yake ulitokana na malalamiko makubwa ya wananchi kuhusu utendakazi wa mawaziri wake. Maandamano ya Gen Z yaliweka shinikizo kubwa kwa serikali, yakihimiza uwajibikaji na uwazi serikalini.
Katika hotuba yake ya Juni 2024, Rais Ruto alisema kuwa kuvunjwa kwa baraza la mawaziri kulilenga kuongeza uwajibikaji, ufanisi na uwazi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Alisema pia kuwa serikali mpya ingekuwa na sura ya taifa kwa kujumuisha viongozi kutoka mirengo mbalimbali ya kisiasa, ikiwa ni hatua ya kuleta mshikamano wa kitaifa.
"Tangu siku hiyo, nimemtazamia Mungu. Sasa mimi nafanya ukulima, sina kazi, napanda na kuuza kabeji huko Cheranganyi," aliongeza.
Licha ya kupoteza nafasi yake serikalini, Nakhumicha anasema anaendelea na maisha yake kama mkulima, huku akitazama mustakabali wake kisiasa.
Haijabainika ikiwa ana mipango ya kurejea kwenye ulingo wa siasa, lakini kwa sasa, anasema anajikita zaidi katika shughuli zake za kilimo.