
Waziri wa Afya Deborah Barasa ameomba msamaha hadharani kwa Bi Grace Njoki, mwanamke aliyekatiza mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu changamoto za Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).
Akizungumza kwenye mahojiano na Citizen TV siku ya Alhamisi, Waziri pia alikanusha kuhusika na kukamatwa kwake.
Barasa alisisitiza kuwa hakuwa na uhusiano wowote na kukamatwa kwa Njoki na akaeleza masikitiko yake kuhusu mateso aliyoyapitia.
"Huenda anatazama runinga sasa, na nataka kumwambia pole kwa yaliyomtokea," alisema Barasa.
Pia alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Wizara ya Afya ina dhamira ya kuwahudumia wananchi.
"Mtazamo wetu ni kuangazia wagonjwa kwanza, maana sisi kama maafisa wa serikali tuko hapa kwa ajili ya kuwahudumia Wakenya. Tumekabidhiwa jukumu hili, na ni lazima tusikilize changamoto zao," aliongeza.
Barasa alisisitiza kuwa wizara yake ina jukumu la kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi.
"Tunapaswa kusikiliza sauti za wananchi na kutatua matatizo wanayokumbana nayo," alisema.
Hata hivyo, wakati wa kikao na wabunge mjini Naivasha mnamo Januari 30, 2025, Katibu wa Huduma za Matibabu, Harry Kimtai, alikiri kuwa Wizara ya Afya (MoH) ndiyo iliyopeleka malalamiko dhidi ya Njoki.
"Wizara iliwasilisha kesi hiyo ikidai Njoki alihusika na kuingia bila idhini na kusababisha vurugu," Kimtai aliwaambia wabunge.
Licha ya hayo, alihakikishia bunge kuwa kwa maslahi ya taswira ya wizara na kudumisha imani ya umma, malalamiko hayo yatafutwa.
Awali, taarifa kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI)
ilieleza kuwa Njoki alikamatwa kwa kosa la kusababisha vurugu ndani ya Ukumbi
wa Bodi ya Wizara ya Afya katika Afya House.
Kukamatwa kwa Njoki kulizua maswali miongoni mwa wabunge, huku Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah, akitaka kujua nani aliyeidhinisha kesi hiyo na kosa mahsusi alilofanya Njoki.
Njoki alikuwa miongoni mwa wagonjwa waliofika katika ofisi za Wizara ya Afya mnamo Januari 15, 2025, wakipinga changamoto zinazoikumba SHA.
Baadaye, aliingia ghafla kwenye mkutano wa Waziri Barasa na waandishi wa habari, akidai mabadiliko ya haraka katika sekta ya afya.
Baada ya tukio hilo, Njoki alikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana ya polisi ya Sh10,000.
Kesi yake imeibua upya mjadala kuhusu ufanisi wa SHA na jinsi serikali inavyoshughulikia malalamiko ya umma kuhusu upatikanaji wa huduma za afya na utawala wa sekta hiyo.