
KINARA wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amekanusha vikali tetesi zinazoenezwa kwamba amekutana na rais William Ruto.
Hii ni baada ya video kienezwa ikimuonyesha Kalonzo na Ruto wakiwa pamoja katika ikulu ya Nairobi.
Kalonzo kupitia kurasa zake mitandaoni, aliitaja video hiyo kuwa feki akisisitiza hawezi kuungana na Ruto.
Kiongozi huyo ambaye amesalia kuwa sauti ya upinzani baada ya Raila kuungana na serikali alisema kwamba hawezi wasaliti wananchi.
“Mbona wana hofu sana? Muungano wa People’s Loyal Coalition hautawahi kuwa chama cha usaliti mkubwa zaidi wa Wakenya kwa manufaa ya kisiasa na faraja ya muda,” alisema.
Kalonzo alisema zaidi kwamba video hiyo iliundwa Machi 9, 2024, wakati wa kuwasilisha ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) katika Ikulu.
Kulingana na Kalonzo, ni jaribio la kutaka kumharibia sifa na kuzua migawanyiko ndani ya mapatano yake ya kisiasa na Martha Karua, Eugene Wamalwa na Rigathi Gachagua.
Mwandani huyo wa miaka mingi na Raila Odinga amekuwa mstari wa mbele kumkosoa kwa kuungana na Ruto.
Kwa mujibu wa Kalonzo, hatua ya Raila Odinga kuungana na Ruto pasi na kuulizia haki ya vijana wa Gen Z waliouawa mwaka Jana ni usaliti mkubwa kwa wananchi.
Yeye na wenzake kama Eugene Wamalwa wa DAP-K, Martha Karua wa PLP na Morara Kebaso wa INJECT wameibuka kuwa wakosoaji wakubwa wa muungano kati ya ODM na UDA.
ODM na UDA vilitia Saini ya makubaliano ya kufanya kazi pamoja Ijumaa iliyopita katika kile baadhi wanahisi ni hatua ya usaliti kwa ODM kuungana na UDA.