
KATIBU mkuu wa muungano wa wafanyikazi humu nchini COTU, Francis Atwoli ametaka watumizi wa mitandao ya kijamii kupunguza kasi ya kile alichokitaja kama kueneza propaganda na siasa za chuki kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii humu nchini.
Akizungumza katika mkutano wa wajumbe wa
COTU Jumamosi, Atwoli alisema kwamba nchi nyingi tu za Afrika zinatamani
utulivu na amani iliyoko Kenya, akionya kwamba watumizi wa mitandao ya kijamii
wanataka kuharibu sifa hiyo zuri ya taifa.
“Kenya ni setellite ya shughuli za
kiuchumi katika kanda hii, hata tukipiga kelele, wale wenzetu Tanzania, Uganda
wanataka Kenya sana kwa sababu ya mifumo ya mawasiliano tuliyo nayo.”
“Sasa viwanda haviwezi kuhama na
hapa ndio kuna kila kitu, isipokuwa kitu naomba tu wale watu wetu wa mitandao
ya kijamii, itabidi mpunguze propaganda. Ni lazima mpende nchi hii, msipopenda
nchi hii waajiri watahama, ama kama si hivyo mtaanza kulimana, mkianza kupigana
tunakuwa kama wenzetu Sudani, Kongo, Somalia na wengine,”
Atwoli alisema.
Kiongozi huyo alisema kuwa ikiwa watumizi
wa mitandao ya kijamii wasipopunguza kasi ya kueneza propaganda itabidi wao
kama muungano wa wafanyikazi wameiandikia serikali barua ya kutaka kudhibitiwa
kwa shughuli za mitandaoni kwa Wakenya.
Alisema kwamba mataifa Tajiri kama vile
China na mengine yamedhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii na hiyo ndio
salama ikiwa matumizi yake yatakuwa yanatishia usalama wa nchi.
“Hatutaki kuenda njia kama ya hayo
mataifa yenye mizozo, lakini watu wa mitandao ya kijamii wanatuelekeza huko.
Unajua sasa itabidi, na hatukutaka hivyo, itabidi tuulize serikali idhibiti
mitandao ya kijamii,” alitishia.
“Kama China wamedhibiti, TikTok ya
China ni yao, sio hii yenu hapa, mambo ya WhatsApp hakuna China, Dubai, Cuba na
hizi nchi zingine. Na ni lazima tuulize kwa sababu ukifungua TikTok siku hizi
na Watoto wadogo wanajua kufungua, mambo mengine yanafanyika huko sijui kama ni
mimi naona pekee,” aliongeza.
Alisisitiza akisema kuwa ikiwa mienendo
hiyo chafu itaendelea basi Suluhu litakuwa kudhibitiwa kwa matumizi ya Wakenya
kwenye mitandao ya kijamii.