
RAIS William Ruto amemiminia sifa dhehebu la AIPCA akidai kwamba ndilo kanisa pekee ambalo limesimama na kupigania serikali kwa muda mrefu.
Akizungumza Alhamisi katika kanisa la AIPCA
jimbo la Meru katika sherehe ya mafuta matakatifu, Ruto alisema kwamba yeye ni
mmoja wa wanufaikaji wakubwa kutokana na mafuta hayo.
Alikumbuka kwamba kabla ya uchaguzi wa 2022,
alihudhuria hafla ya Holy Oil ya kanisa la AIPCA kaunti ya Nyeri na wiki chache
baadae akatwaa urais.
“Hili ndilo kanisa la serikali. Mimi
ningependa kutoa shukrani kwenu, hii Holy Oil, kabla hatujaenda uchaguzi 2022,
nyinyi mnajua tulikuwa pale Nyeri, na nilikuja pale. Na kwa sababu ya maombi
yenu na haya mafuta ya Holy Oil, si mimi ni rais wa Jamhuri ya Kenya leo? Si Bwana
Yesu asifiwe jamani?”
“Mimi ni mnufaikaji na ningependa
kuwaambia kwamba kwa sababu hii na maombi yenu, na mwenyekiti wetu mama hapa
amesema mnaombea taifa letu la Kenya na mnaiombea pia. Wakati mwingine hamjui
kama hayo maombi yanafika ama hayafiki. Wacha niwape hakikisho kwamba maombi
mnaoniombea yanafika,” Ruto alisema.
Kiongozi wa taifa aliradidi kwamba anaendelea
kupata nguvu ya kuchapa kazi kutokana na maombi ya Wakristo na haswa wale wa
dhehebu la AIPCA.
“Nataka tu niwahakikishie kwamba hiyo
kazi mliyonipatia kwa maombi yenu nak wa kura zenu, mimi nitafanya kwa bidii na
kwa kujitolea. Na itafanyika, na tutamuaibisha shetani, mimi ndio nawaambia,” alisema.
Ruto alimaliza kwa kuomba msaada wa kanisa la
AIPCA ambalo alidai yeye ni mshirika wake wa muda mrefu, kumsaidia kuunganisha Wakenya
wote.
“Askofu, wewe ndiye kiongozi wetu wa
kanisa hili na mimi ni member wa hili kanisa, nimesema mnisaidie tuunganishe
taifa letu la Kenya. Na chochote kitakachohitajika, mimi kama kiongozi wa taifa
hili nitafanya ili kuunganisha wananchi wote wa taifa hili,”
Ruto alisema.
Katika ibada hiyo pia, kiongozi wa taifa
alizidi kutetea serikali jumuishi akisema kwamba ni pana kiasi kwamba inaweza
kujumuisha kila mmoja Kenya yote na si lazima mmoja aondoke ili kutengenezea
mwingine nafasi.