
KATIBU mkuu wa muda mrefu wa muungano wa wafanyakazi humu nchini COTU, Francis Atwoli amedokeza kwamba huenda muda wake katika usukani huo unayoyoma na hivi karibuni atastaafu.
Haya ni kwa mujibu wa Kauli yake
aliyoitoa katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa mlinzi wa Raila Odinga, George
Oduor.
Akizungumza katika mazishi hayo
Jumamosi katika kaunti ya Siaya, Atwoli alisema kwamba amefanya kazi chini ya
kila serikali ya Kenya tangu kupatikana kwa uhuru mwaka wa 1963.
Mzee huyo alisema kwamba amefanya kazi
chini ya marais wote ambao Kenya imekuwa nao tangu hayati Mzee Kenyatta, Moi,
Kibaki, Uhuru na sasa chini ya rais William Ruto.
Hata hivyo, alidokeza kwamba huenda
serikali ya Ruto ikawa ya mwisho kwake kufanya kazi nayo kabla ya kustaafu na
kurudi nyumbani kwake Khwisero, kaunti ya Kakamega.
“Mimi nimepata nafasi ya kuhudumu chini
ya marais wote wa Kenya tangu kupatikana kwa uhuru. Nimeona serikali ya
Kenyatta – mzee Mwanzilishi wa taifa hili, nimeona serikali ya Moi ambaye
tulikaa naye kwa miaka 24, nimeona serikali ya Kibaki, nimeona serikali ya
Uhuru na nimeona serikali ya Ruto. Na labda serikali hii ndio itakuwa ya mwisho
halafu nirudi kule Khwisero,” Atwoli alisema.
Atwoli amehudumu kama Katibu Mkuu wa
COTU kwa zaidi ya miongo miwili. Alichukua wadhifa huo mnamo Agosti 2001 na
tangu wakati huo amekuwa akifanya kazi katika harakati za wafanyikazi, ambapo
amechaguliwa tena mara nyingi.
Hata hivyo, katika siku za hivi
karibuni, kumekuwa na mjadala baadhi ya watumizi wa mitandao ya kijamii
wakihoji ni lini Atwoli atang’atuka kama katibu wa COTU.
Mmoja wa watu ambao wametilia shaka
kukaa kwa muda mrefu kwa Atwoli afisini ni aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya
Makueni Kivutha Kibwana, ambaye, huku akimpongeza Atwoli kwa kuzaliwa kwa mtoto
wake wa hivi punde, alimpa changamoto ya kufikiria kustaafu.