
Naibu Rais Kithure Kindiki amesema haoni tatizo lolote na tabia yake ya kumjibu Rais William Ruto kwa maneno ya "Yes Sir!"
Akizungumza katika hafla ya uwezeshaji huko Hola, Kaunti ya Tana River, siku ya Jumatano, Julai 2, 2025, Kindiki alisisitiza kuwa ataendelea kuwa mtiifu kwa Rais Ruto.
Kindiki pia alimkosoa yeyote anayepinga uaminifu wake kwa rais, akidokeza kuwa hiyo ndiyo chanzo cha matatizo ya kisiasa ya baadhi yao.
“Wacha niwaulize, kuna shida gani kuwa mtu wa ‘ndiyo mheshimiwa’ kwa rais? Hata Joho humwambia rais, Ndiyo mheshimiwa. Sivyo inavyopaswa kuwa?” aliuliza.
“Wale wengine wenye maringo wanapaswa kukumbushwa kwamba walikosa kufanya hivyo, na ndiyo sababu sasa wamesahaulika,” aliongeza.
“Kile hawajui ni kuwa mimi pia huwaambia wananchi, ‘Ndiyo mheshimiwa,’ kwa sababu wao ndio waajiri wetu sote, hata rais,” alieleza.
Kauli hizi zinakuja baada ya Seneta wa Tana River, Danson Mungatana, kumkosoa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa siasa zake za kugawanya taifa alipokuwa akihudumu kama Naibu Rais wa pili wa Kenya.
Akizungumza katika hafla hiyo hiyo, Seneta Mungatana alilenga ukosoaji wake kwa Gachagua, akimtaja kuwa fedheha ya kitaifa wakati wa kipindi chake ofisini.
“Sasa tumemkubali Kindiki kama jirani mwema ambaye ametutembelea mara nyingi. Pia yeye ni Naibu Rais anayefaa na anayestahili.
Yule wa awali alikuwa fedheha kwa urais. Alikuwa akidai kuwa ukanda wa Pwani hauko katika mipango yake, na kadhalika. Mipango yake ilikuwa tu kwa ajili ya watu wa eneo lake la nyumbani,” alisema.
“Ndiyo sababu tulisema tutamwondoa na kumdhibiti, lakini Mwengi Mutuse akaja na hoja iliyomng’oa mamlakani.
Tunataka kuijenga Kenya iliyoungana, lakini Wamunyoro alitaka kutufunga kwa minyororo ya ukabila.
Ndiyo maana sasa tumeungana na tunasonga pamoja kama viongozi wa Pwani,” alisema aliyekuwa Mbunge wa Garsen.