
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amewasifu polisi kwa jinsi walivyodhibiti waandamanaji wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba siku ya Jumatatu.
Murkomen alisema maafisa wa usalama walijizuia na kuonyesha nidhamu katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Nilikagua Jiji la Nairobi kuwashukuru maafisa wetu wa usalama waliokuwa kazini kuhakikisha usalama wa wananchi wetu na mali zao,” Murkomen alisema.
“Kwa sababu ya juhudi zao na za maafisa wengine kote nchini, visa vya ghasia, uporaji na uharibifu wa mali vilipungua kwa kiasi kikubwa leo ikilinganishwa na wiki iliyopita. Tumejizatiti kuhakikisha maandamano yanakuwa ya amani na ya mpangilio,” aliongeza.
Murkomen pia alitetea hatua ya kuzuilia ufikiaji wa katikati mwa jiji la Nairobi (CBD) siku ya Saba Saba, akisema ilikuwa ya kulinda biashara na wananchi dhidi ya wahuni waliokuwa wakivamia maandamano yaliyopita.
Asubuhi ya Jumatatu, barabara kadhaa zinazoelekea CBD ya Nairobi zilifungwa, hali iliyowalazimu madereva kutafuta njia mbadala kufika walikokuwa wakielekea.
Hatua hiyo pia ilisababisha maelfu ya wasafiri wa masafa marefu kukwama kwa sababu hawakuweza kufika katikati mwa jiji ili kuendelea na safari zao.
Hata hivyo, Murkomen aliomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza, akisisitiza kuwa ilikuwa kwa nia njema na malengo yao yalikuwa chanya.
“Kwa sababu ya mikakati tuliyoweka leo, wahuni na wahalifu wengi hawakupata nafasi ya kuvamia mali ya watu. Hata hivyo, Wakenya wengi walipata usumbufu — wengine walishindwa kufika ofisini, wengine kwa hofu ya kilichotokea wiki iliyopita walikataa kufungua biashara.
"Kwa hivyo, ningependa kuwaambia Wakenya waliokumbwa na usumbufu kutokana na operesheni za kiusalama, poleni sana. Tulilazimika kufanya hivyo kwa sababu tungependa nyinyi pamoja na mali yenu muwe salama,” Murkomen alisema.
“Malengo yetu ni chanya, nia yetu ni kuokoa maisha na kulinda mali ya Wakenya. Kila Mkenya anapaswa kuwa nyumbani akiwa na furaha kwa sababu, kadri ya uwezo wetu, Huduma ya Kitaifa ya Polisi pamoja na maafisa wa polisi wamepunguza uharibifu leo.”
Hata hivyo, alisema kuna matukio yaliyoripotiwa ambapo wahuni walipora maduka na majengo kuchomwa.
Alisema polisi watachunguza matukio yote yaliyohusiana na maandamano ya kuadhimisha Siku ya Saba Saba na kuchukua hatua zinazofaa.
Waziri huyo aliendelea kuwasifu polisi, akisema walifanya kazi nzuri ya kuwalinda Wakenya na mali zao.
“Asanteni sana kwa sababu kama isingekuwa kazi yenu, tungekuwa tunajadili aina ya uharibifu tuliouona wiki iliyopita. Kwa hivyo, tunapokaribia mwisho wa siku, nilihisi ni muhimu sisi kama timu kutoka wizara kuja kusema asanteni nyote. Najua si nyinyi peke yenu, kuna maafisa kote nchini waliotoa huduma bora kwa kudhibiti wahalifu na wahuni waliokuwa wakivuruga maandamano ya amani ya raia,” alisema.
Murkomen aliongeza kuwa polisi wamefanya kazi nzuri katika kuvunja maandamano tofauti na ghasia zilizoshuhudiwa katika maandamano yaliyopita.
Waziri huyo pia alisema kuwa washukiwa waliokuwa na ushiriki katika maandamano ya Juni 25, 2025, yaliyosababisha ghasia, wamekamatwa.